Na Abby Nkungu, Singida
ELIMU na hamasa kwa wazazi juu ya umuhimu wa kusomesha watoto wenye mahitaji maalumu imeanza kuzaa matunda katika Manispaa ya Singida baada ya idadi ya wanafunzi walioandikishwa kuanza masomo ya Awali na darasa la Kwanza mwaka huu kuongezeka kwa asilimia 30.
Takwimu kutoka kwa Afisa elimu msingi Manispaa ya Singida, Omary Maje zinaonesha kuwa jumla ya watoto 84 wenye mahitaji maalumu wamesajiliwa kwenye shule na vitengo mbalimbali vilivyopo kwa ajili ya kuanza masomo ya Awali na Msingi mwaka huu 2023.
“Idadi hiyo ya uandikishaji watoto wenye mahitaji maalumu ni sawa na ongezeko la asilimia 30 ikilinganishwa na mwaka jana; hivyo kuonesha dhana potofu katika jamii kupungua na sasa wanawapeleka shule watoto wao badala ya kuwaficha majumbani kama ilivyokuwa hapo awali” alisema.
Alifafanua kuwa miongoni mwa watoto hao walio na umri wa miaka minne hadi sita, 61 wapo kwenye hatua ya kwanza ya masomo, 10 elimu ya awali na 13 wameanza darasa la kwanza.
“Siku za nyuma ilikuwa vigumu sana kuandikisha idadi hiyo ya watoto kutokana na baadhi ya wazazi kuwaficha majumbani kwa kuona aibu au fedheha lakini baada ya kuanza kwa Programu Jumuishi ya Taifa juu ya Malezi, Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto (PJT- MMMAM) Januari mwaka 2021, kumekuwa na mwamko mkubwa wa kusomesha wenye mahitaji maalumu” alieleza.
Alisema kuwa chini ya Programu hiyo inayohusu afya bora, lishe, malezi yenye mwitikio, fursa za ujifunzaji wa awali, ulinzi na usalama na sekta nyingine mtambuka, Viongozi na Watendaji wa mitaa wamekuwa wakitembelea maeneo yao kubaini watoto hao huku wakitoa elimu juu ya umuhimu wa kuwasomesha.
Maje alisema kuwa katika Manispaa hiyo, wapo walimu wa kutosha wa kufundisha elimu maalumu kwenye vitengo na shule Jumuishi lakini akakiri kuwa bado kuna changamoto ya vifaa vya kujifunzia na kufundishia pamoja na miundombinu duni kwa ajili ya kundi hilo muhimu.
“Walimu wapo 26 ila vifaa vya kufundishia na kujifunzia havipo vya kutosha na mwaka jana tumeongeza vitengo viwili kwa ajili ya watoto wenye ulemavu wa akili ambavyo bado havina zana muhimu. Hata vile vya zamani havina uzio, madarasa wala vyoo maalumu kwa wenye mahitaji maalumu lakini juhudi za kuboresha zinazofanyika".
Mmoja wa walimu wa elimu maalumu ambaye hakupenda jina lake litajwe, pamoja na kukiri kuwepo kwa maboresho alisema changamoto bado kubwa; hasa kwa wale wanaosoma kwenye shule Jumuishi kwani hakuna vifaa vya kutosha wala miundombinu maalumu kwa kundi hilo.
“Hawa wenye ualbino wana uoni hafifu hivyo wanatakiwa kupewa miwani maalumu kwa ajili ya kusomea….hawana. Mafuta maalumu ya kupaka ngozi nayo hakuna. Kwa wasioona, hakuna vibao vya nukta nundu na hapo hujagusa vyoo na mahitaji mengine muhimu” alisema kisha akaiomba Serikali kuendelea kuwaangalia kwa jicho la pekee ili wasome kama wengine.
Baadhi ya wazazi na walezi wanasema kutokuwepo kwa vifaa au zana za kujifunzia na kufundishia na miundombinu rafiki kwa watoto hao ni miongoni mwa sababu zinazowafanya wazazi wengine kuwaficha watoto wao wakidhani kuwa wataenda kuteseka zaidi huko shuleni.
“Hebu fikiria mtoto wako anatembea kwa mikono halafu unaambiwa aende shule ambayo haina choo maalumu, wewe kama mzazi wake utakubali?” alihoiji Halima Ali mkazi wa Kibaoni Singida mjini huku Lazaro Lameck (70) mkazi wa Mtaa wa Salmin akisema njia pekee ni kuboresha zaidi shule za watoto wenye mahitaji maalumu ili zivutie wazazi.
Sera ya elimu Jumuishi ya mwaka 2014, inataka watoto wenye ulemavu, wenye mahitaji maalumu na waliopo kwenye mazingira magumu kusoma pamoja na wenzao wa kawaida kwenye shule moja bila kubaguliwa ili kumwezesha kila mtoto wa kitanzania kupata haki ya elimu bila kikwazo chochote.
.
Post A Comment: