Na;Elizabeth Paulo, Dodoma

Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) katika kutatua changamoto za kukata kwa umeme mara kwa mara imeanzisha programu ya Gridi Imara ambapo mradi utagarimu jumla ya shilingi Trilioni 4 na katika mwaka wa fedha 2022/2023 serikali ya awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan imetoa kiasi cha shilingi milioni 500.


Shirika linatekeleza ilani ya chama cha Mapinduzi ya kufikisha uzalishaji wa megawat 5000 za kuingizwa katika Gridi ya Taifa kufikia 2025 ambapo uzalishaji wa sasa ni megawat 1820 na mitambo iliyopo huzalisha megawat 1300.


Kaimu Mkurugenzi Huduma kwa Wateja (TANESCO) Marthin Mwambene amesema hayo leo jijini Dodoma wakati akielezea utekelezaji wa majukumu ya Shirika mbele ya Waandishi wa habari.


TANESCO ina miradi mbadala ambayo itaongeza uwezo wa uzalishaji wa umeme ikiwemo ya gesi na jua, pia kuna vyanzo binafsi vyenye uwezo wa kuzalisha umeme mfano viwanda vya sukari.


Mradi wa Umeme wa bwawa la Julius Nyerere utaingiza megawat 2,115 Ambapo mpaka sasa mradi umefika asilimia 88 na unatajajiwa kukamilika 2024.



“Kama TANESCO tumejipanga kutatua changamoto za wananchi kwa kuanzisha mpango huu wa Gridi Imara na Tunakwenda kumalizia tatizo la kukatika kwa ummm. ”Alisema Mwambene


Aidha Miradi ya uzalishaji umeme inaenda sambamba na miradi ya kusafirisha umeme, katika mradi wa JNHPP kuna njia ya kusafirisha umeme itakayoanzia Rufiji mpaka Chalinze na tayari transfoma kubwa takriban sita zimepelekwa zinasubiri kufungwa.


“Kuna baadhi ya mikoa ikiwemo Rukwa na Katavi haipo katika Gridi ya Taifa, hivyo kuna laini ambazo zitajengwa ambazo zitakuwa zinaunganisha nchi na nchi nyingine, Karibu nchi nzima itakuwa ipo katika mfumo wa Gridi ya Taifa.”Alisema 


Mradi wa Gridi Imara utajumuisha ununuzi wa mashine umba 6,000, mita laki 7 za umeme, nguzo 380,000, ununuzi na ufungaji wa nyaya zenye urefu wa KM 40,000, ujenzi wa vituo 14 vya kupoza umeme na ujenzi wa njia za kusafirisha umeme mkubwa takriban KM 948.


“Mradi huu wa Gridi Imara ni ushahidi kwamba matatizo ya umeme yaliyopo nchini tunayafahamu na tunatarajia mradi huu utayatatua.”Alisema na Kuongeza


“TANESCO haiuzi nguzo bali inauza huduma ya umeme. Aidha, inapothibitika kuwa nyumba iliyoungua imesababishwa na umeme, fidia huwa zinalipwa.”


Mwambwene Amesema Shirika limeanzisha kituo cha kupokea changamoto za wananchi kwa kupiga simu ili kuwasaidia wananchi kupata huduma bila kufika ofisi za TANESCO.





“Tumevunja ule utendaji kazi wa kujuana na kuanzisha mpango huu lazima tuwasaidie wananchi ndio maana tumeanzisha kituo hiki.”Alisema Mwambene


Kwa upande wake Meneja Mawasiliano na Uhusiano kwa Wadau Elihuruma Ngowi Amesema mwaka 2022 Shirika lilianzisha kampeni maalumu ya kutoa elimu kwa wananchi kupitia vyombo mbalimbali vya habari kuhusiana na athari zinazoweza kujitokeza baada ya miundombinu ya Umeme Kuathiriwa.


“Tunaendelea kufanya zoezi hili la kutoa elimu kwa wadau na ni zoezi endelevu na tunahakikisha tunafanya kila wakati, tunao Maafisa wa usalama ambao wanatusaidia kuhakikisha kwamba wanatoa elimu kwa wadau wote”.Alisema Ngowi


Share To:

ELIZA DOM

Post A Comment: