Na Dotto Mwaibale, Dodoma
MFUMO wa ununuzi wa mazao kwa njia ya mtandao unaoendeshwa na Soko la Bidhaa Tanzania (TMX) umesaidia kupandisha bei ya mazao ya wakulima ambayo uuzwa kwa mnada.
Hayo yamebainishwa na Afisa wa Teknolojia ya Habari na Mawasilino (TEHAMA) kutoka TMX, Goodluck Luhanjo wakati akizungumza katika mafunzo yaliyokuwa yakitolewa kwa waandishi wa habari wa mikoa ya Dodoma na Singida kuhusu shughuli mbalimbali zinazofanywa na taasisi hiyo iliyo chini ya Wizara ya Fedha na Mipango.
Alisema katika kipindi cha kuanzia mwaka 2018 hadi 2022 TMX imefanikiwa kuuzwa kwa tani 107,056,619 za bidhaa mbalimbali zenye thamani ya Sh. Bilioni 223.26 na kati ya fedha hizo Sh. Bilioni 212.09 sawa na asilimia 95 zililipwa kwa wakulima na kutaja mazao yaliyouzwa kuwa ni ufuta, choroko, korosho, kakao, kahawa na dengu.
Akitolea mfano alisema kabla ya kuanzishwa kwa mfumo huo wakulima walikuwa wakiuza choroka kwa Sh.400 hadi 900 lakini baada ya kuanza kuuza kwa kutumia mfumo huo bei imepanda hadi kufikia Sh.1340,huku zao la kokoa katika mikoa ya Tanga, Mbeya na Morogoro iliyokuwa ikiuzwa kwa Sh.1200 ikipaa hadi kufikia Sh.4500 hadi 5000 kwa kilo baada ya kuuzwa kwa mfumo huo.
"Tulivyofanya tathmini kwenye mnyororo wa thamani wa zao la ufuta wilayani Kondoa mkoani Dodoma na Babati mkoani Manyara ulikuwa ukiuzwa kati ya Sh. 1200 hadi 1500 lakini baada ya kuingia kwenye mfumo bei ilipanda hadi kufikia Sh.3,195 kwa kilo moja" alisema Luhanjo.
Akizungumzia zao la kahawa mkoani Kagera alisema kwa msimu wa mwaka jana kahawa aina ya robosta ambayo ilikuwa haijabanguliwa maganda ilikuwa ikiuzwa kati ya Sh.900 hadi 1200 lakini baada ya kuuzwa kwa njia ya mfumo bei ilipanda hadi kufikia Sh.2000 hadi 2500 kwa kilo.
Meneja Uendeshaji Biashara wa TMX, Augustino Mbulumi, akizungumzia faida kadhaa za soko la bidhaa Tanzania alisema ni kuimarisha bei kwenye soko,kupunguza hatari ya upotoshaji wa soko, upatikanaji wa taarifa za Soko na uhakika wa malipo kwa wakulima.
Alitaja faida nyingine kuwa ni kupunguza gharama muda na fedha, kupunguza athari mbalimbali kwenye ubora na wizi, uwezo wa kupata mazao mengi na yenye ubora kwa wakati mmoja na imesaidia biashara ya kimataifa kwa gharama nafuu.
Aidha, Mbulumi alisema kwa upande wa Serikali inasaidia upatikanaji wa taarifa ya kuaminika, njia rahisi za kukusanya mapato, bodi za mazao zinaweze kujikita katika uzalishaji wa mazao na kuhamasisha kampeni ya uchumi wa viwanda.
Alitaja baadhi ya changamoto kuwa ni zile za kimiundombinu kuwepo kwa maghala machache yanayozingatia viwango vya kuhifadhi mazao hasa nafaka, vifaa vichache au kukosekana kabisa kwenye baadhi ya maeneo ya minada ya mifugo.
Alitaja changamoto nyingine kuwa ni upinzani kutoka kwa baadhi ya wafanyabiashara ambao walikuwawakinufaika sana na biashara isiyo rasmi, kuwepo kwa mgongano wa maslahi na wakati mwingine husababisha upinzani wa mabadiliko, vyama vya ushirika kuzoea kutumia 'sanduku la zabuni’ na njia zisizo za kidijitali hivyo kuwepo na upinzani wa kutumia mfumo waKielektroniki wa Soko la Bidha.
"Baadhi ya hatua zilizochukuliwa kukabiliana na changamoto hizi ni kupitia Wizara ya Kilimo, na kufanya kazi na Bodi ya Stakabadhi za Ghala, kuna mipango ya kuwa na ghala katika ngazi ya wilaya kwenye maeneo ya uzalishaji, Wizara ya Mifugo na Uvuvi tayari imeanza mchakato wa kuhuisha vifaa hivyo hasa mashine za kupimia mifugo uzito na kupata vifaa vinavyohitajika katika maeneo ya minada kuboresha utendaji kazi." alisema Mbulumi.
Post A Comment: