Wafanya usafi zaidi ya 70 wanaosafisha mitaa ya jiji la Mwanza wameandamana hadi ofisi za kampuni ya Green Waste kudai malimbikizo ya mishahara ya miezi sita.
Pamoja na madai ya mishahara, wafanya usafi hao waliobeba mabango kadhaa yenye ujumbe wa kuomba msaada ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana na uongozi wa jiji pia wanadai kurejeshewa Sh15, 000 wanazokatwa kila mwezi bila kuwasilishwa Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF).
Juhusu za kuupata uongozi wa Green Waste kujibu madai hayo hazikufanikiwa baada ya mwandishi wa habari kufika ofisini kwao na kukuta ofisi imefungwa na kwenye simu hakupatikana.
Akizungumza na waandishi wa habari nje ya ofisi za Green Waste zilizoko barabara ya Kenyatta zilizokuwa zimefungwa leo Januari 31, mmoja wa wafanyausafi hao, Amina James (69) amedai kuzunguzwa na kampuni hiyo kila anapofuatilia madai yake.
“Mimi kwa mwezi nalipwa 120,000 lakini sasa hela hatuna nafanya kazi kama sifanyi kazi mshahara sipati nikija kwa bosi wangu ananiambia hana hela na kuniambia niende popote pale ninapotaka.
“Ukiendelea kumdai anasema yeye anadai jiji bado hawampa hela, sasa nashindwa nifanyaje naomba viongozi mtusaidie na kutuonea huruma,” amesema Amina.
Naye Edward Cheye, Mkazi wa Bugarika amesema amesema hali hiyo imemfanya maisha kuwa magumu zaidi na kushindwa kuwahudumia watoto wake na kuwapeleka shuleni.
“Mpaka saizi watoto wanahangaika hawajaenda shule hata nguo hawana lakini nikija huku kudai haki yangu sipati na naambulia majibu mabaya, namuomba Rais Samia Suluhu Hassan, Mkuu wa Mkoa na Mkuu wa Wilaya watusaidie tupate haki zetu,” amesema Cheye.
John Kennedy, Mfanyausafi katika jiji hilo amesema pia wanadai kuingiziwa fedha kwenye mfuko wa NSSF ambazo tangu 2017 kampuni hilo halijafanya hivyo huku kila mwezi wakikatwa 15,000.
“Tangu mwezi Machi 2017 nilianza kukatwa kwenye mshahara wangu fedha ya NSSF lakini ukienda kuangalia kwenye akaunti yangu hamna hela, ukimuuliza mhasibu anakwambia hajapeleka na hela yupo nazo ndani,” amesema Kennedy.
Alipoulizwa kuhusu suala hilo, Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana, Amina Makilagi amesema analifahamu na anawasiliana na mamlaka husika kuona namna ya kuvunja mkataba wa tenda hiyo kutokana na kushindwa kutimiza masharti ya mkataba.
“Madai hayo niliyapokea na niseme tu kampuni hilo halifai kufanyakazi katika Mkoa wa Mwanza na Tanzania kwa ujumla kwa sababu imeshindwa kutekeleza masharti mkataba na hawazingatii maslai ya wafanyakazi.
“Anakusanya mapato bila kupeleka kwenye mfuko wa serikali, kwahiyo sasa kwa vile tulisaini mkataba naye hapa tunafanya utaratibu wa kuvunja,” amesema Mwakilagi.
Hata hivyo, Mwakilagi amewasihi wafanyausafi hao kutekeleza agizo lake la kuifuata mamlaka inayohusika na kazi ili wapate stahiki zao ambazo wamekuwa wakidai kwa wakala huyo
Post A Comment: