Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Sophia Mjema ameutaka uongozi wa Mkoa wa Tanga kuhakikisha hospitali ya Wilaya ya Handeni inaanza kutoa huduma ifikapo mwishoni mwa mwezi huu.
Agizo hilo amelitoa leo wakati wa ziara ya wajumbe wa sekretarieti ya Halmashauri Kuu Taifa ya CCM mkoani Tanga. ambayo imelenga kukagua utekelezaji wa ilani ya chama hicho sambamba na kuimarisha uhai wa Chama.
Amesema kutokana na hatua iliyofikiwa ya maendeleo ya ujenzi wa hospitali hiyo, haoni ucheleweshaji wa huduma hadi kufikia Machi 30 mwaka huu, kwani wananchi wa Handeni wana uhitaji wa huduma karibu na eneo lao badala ya kutembelea umbali mrefu.
“Niwaagize uongozi wa mkoa uwekezaji uliofanyika katika hospitali hii ni mkubwa na wananchi wanasubiri huduma, wakati tukisubiri ujio wa mashine mbalimbali za vipimo ni bora zile huduma za awali ziweze kuanza,”amesema Mjema.
Alisema kuwa serikali ya awamu sita imekuwa ikitumia gharama kubwa kufanya uwekezaji kwenye sekta ya afya, lengo ikiwa ni kupunguza gharama za matibabu kwa wagonjwa kwenda nje ya nchi na badala yake waweze kupatiwa matibabu humu nchini.
Awali akisoma taarifa ya maendeleo ya ujenzi wa mradi wa hospitali hiyo, Mganga Mkuu wa Wilaya ya Handeni Dk Kanansia Shoo amesema kuwa hospitali hiyo inajengwa kwa ushirikiano baina ya serikali ya Tanzania na taasisi ya Islamic Help kwa gharama ya sh Bil 6.
“Tayari majengo ya awali kama vile jengo la wagonjwa wa nje, huduma ya dharura pamoja na wodi ya mama na mtoto yamekamilika kwa ajili ya kutoa huduma, huku serikali ikiwa imeshatuletea watumishi 30 Kwa kuanzia,”amesema Dk Shoo.
Post A Comment: