Kutoka kulia walioketi ni Bw. Emmanuel Ngumbulu (Mwenyekiti wa JTC), Bi. Renatha Mpandaguzi (Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa PURA), Bw. Jaffer Chilala (Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa ZPRA) na Bi. Arafa Rashid (Katibu wa JTC).
************************
Menejimenti za Mamlaka ya Udhibiti Mkondo wa Juu wa Petroli (PURA) ya Tanzania Bara na Mamlaka ya Uthibiti, Utafutaji na Uchimbaji wa Mafuta Zanzibar (ZPRA) ya Zanzibar zimeelezea kuridhishwa na kasi ya utekelezaji wa Hati ya Makubaliano (Memorandum of Understanding - MoU) iliyoingiwa baina ya Taasisi hizo.
Menejimenti hizo imeeleza hayo leo, tarehe 25 Februari 2023 Jijini Dar es Salaam katika kikao kilichohusisha Menejimenti na Timu ya Pamoja ya Wataalamu (Joint Technical Committee - JTC). Kikao hicho kililenga kupokea na kujadili taarifa ya utekelezaji wa MoU kwa robo ya pili ya mwaka wa fedha 2022/23.
“Hakika kazi kubwa imefanyika na sisi kama menejimenti tumeridhishwa na hatua iliyopigwa katika kutekeleza MoU kati ya PURA na ZPRA. Ni matumaini yetu kuwa kasi hii itaendelea zaidi ili tuweze kufikia malengo ya masharikiano tuliyojiwekea” alisema Kaimu Mkurugenzi wa PURA, Bi. Renatha Mpandaguzi wakati akitoa mchango wake kufuatia taarifa iliyowasilishwa.
Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi wa ZPRA, Bw. Jaffer Chilala aliipongeza JTC kwa kujitoa kikamilifu kuhakikisha PURA na ZPRA zinafikia malengo ya yale waliyokubaliana kwenye MoU. “Ingawa tulianza utekelezaji rasmi wa makubaliano mwezi Agosti 2022, inatia moyo kuona mengi yameweza kufanyika ndani ya muda mfupi” alieleza Bw. Chilala.
Mbali na kupokea na kujadili taarifa ya utekelezaji wa MoU, kikao hicho pia kilipokea na kujadili Mpango Kazi na Bajeti ya JTC kwa mwaka wa fedha 2023/24 na Mpango wa Pamoja wa Usimamizi wa Data (Joint Data Management Plan).
PURA na ZPRA zilisaini Hati ya Makubaliano tarehe 19 Februari, 2022. Ili kufanilisha utekelezaji wa MoU hiyo, taasisi hizi ziliunda Timu ya Pamoja ya Wataalamu inayojumuisha wajumbe watano (5) kutoka kila upande.
MoU hiyo inalenga mashirikiano katika maeneo mbalimbali yakiwemo kubadilishana uzoefu katika maandalizi ya kanuni zinazoongoza masuala mkondo wa juu wa petroli, usimamizi wa data za petroli na ukaguzi za mikataba ya uzalishaji na ugawanaji wa mapato.
Post A Comment: