Mchungaji Yona Ezekia wa Kanisa la Moravian Parishi ya Sabasaba mkoani Singida akizungumza na waumini wa kanisa hilo (hawapo pichani) wakati akitoa mafundisho kuhusu namna ya kujikinga na ukatili wa kijinsia dhidi ya watoto na wanawake katika ibada iliyofanyika Jumapili Februari 19, 2023.
Na Dotto Mwaibale, Singida
IMEELEZWA kuwa kukithiri kwa vitendo vya ukatili wa kijinsia kunasababishwa na ugomvi usioisha katika jamii, matumizi ya dawa za kulevya, kulipiza kisasi na msongo wa mawazo.
Hayo yamebainishwa na Mchungaji Yona Ezekia wa Kanisa la Moravian Parishi ya Sabasaba mkoani Singida wakati akitoa mafundisho kuhusu namna ya kujikinga na ukatili wa kijinsia dhidi ya watoto na wanawake katika ibada iliyofanyika Jumapili.
Akimnukuu Mchungaji Revocatus Meza wa Kanisa la Moraviani Jimbo la Rukwa ambaye ni Mthiolojia mbobezi na mtaalamu wa masuala ya ukatili alisema hizo ni baadhi tu ya sababu zinazosababisha matukio hayo ya ukatili.
Alisema katika maandiko yake Mchungaji Meza anasema ukatili wa kijinsia ni kitendo anachokifanya mtu yeyote awe mwanamke au mwanaume kwa lengo la kumdhuru mtu, kumuumiza, kimwili, kisaikolojia, kiafya na kiuchumi.
Alisema Mchungaji Meza anasema zipo aina mbalimbali za ukatili wa kijinsia ukiwepo wa kiuchumi ambao ni kwa mtu kutokuwa na sauti katika mali inayomuhusu,kufanyishwa kazi kwa malipo madogo tofauti na makubaliano na , kutomiliki mali inayomuhusu.
Meza anataja aina nyingine ya ukatili kuwa ni watu kuwasafirisha watoto na wanawake kwenda nje ya nchi kutafuta kazi za ndani na shughuli nyingine ambako wamekuwa wakilipwa ujira mdogo na kufanyiwa vitendo vya kuutweza utu wao.
Mchungaji Meza anautaja ukatili wa kiafya akitolea mfano mama mjamzito kutojaliwa na mume wake, kutopewa fedha za kwenda kliniki, kusaidiwa kazi na kupewa chakula bora kinachoshauriwa na daktari sanjari na mambo mengine yanayofanana na hayo.
Ukatili mwingine uliozungumziwa na Mchungaji Meza ni ukatili wa kimwili kupigana, kuporwa, kudhalilishana na kuwa changamoto nyingi zimekuwa zikisababishwa na ukati huo na hasa kwenye ndoa.
Alisema ukati huo umekuwa ni hamsini kwa hamsini kati ya mume na mke kwani wanaume nao wamekuwa wakipigwa na wake zao na wanawake nao wamekuwa wakipigwa na wanaume zao.
Akitoa mafunzo hayo Mchungaji Ezekia alisema hivi sasa kumekuwa na janga kubwa kwa watoto ambao wanasomeshwa shule za bweni ambapo wazazi wao wamekuwa walinzi na baadhi yao kwenda mbali zaidi hadi kufikia hatua ya kuwakagua kutokana na kukithiri kwa vitendo vya ubakaji na ulawiti.
“Hali hii imekithiri baada ya baadhi ya watu kujitwalia utukufu bila ya kumuogopa Mungu ambapo sasa wazazi na walezi wamefikia hatua ya watoto wao wasikae shule za bweni badala yake wamewatafutia shule za kwenda nakurudi nyumbani” alisema Ezekia
Alisema jambo litakalosaidia kubaini vitendo hivyo kwa watoto, wazazi na walezi waache kuwa bize badala yake wapate muda wa kuzungumza na watoto wao ili kujua changamoto zao pindi watoto wanaporudi nyumbani na kuchunguza mienendo yao.
Mchungaji Ezekia alitumia nafasi hiyo kuwaomba waumini wa kanisa hilo kuwa na moyo wa kujali wengine, kuwa na huruma kwa watu, kujitambua pale wanapokosea, kutowakwaza wengine na kwa kufanya hivyo kutampendeza Mungu na kuachwa kufananishwa na watu wanaowafanyia ukatili wenzao na watoto.
Akitolea mfano katika biblia kitabu cha Marko mstari wa 10 hadi wa 11 alisema Yesu alitambua umuhimu wa watoto na kusema waachwe waende kwake na hivyo hivyo iwe kwa wazazi na walezi kuwatendea wema, kuwaelekeza na kuwashauri badala ya kuwafanyia vitendo vya ukatili vikiwemo kuwachoma moto,kuwabaka na kuwalawiti.
Alisema katika biblia Luka Mtakatifu sura ya 10 mstari wa 31 hadi 33 imeeleza kuwa ukatili ni kutokujali akitolea mfano wa msamaria mwema ambaye alimkuta mtu akiwa amelala barabarani akiwa amejeruhiwa huku watu wakimpita pasipo kumpa msaada wowote.
Aidha, Mchungaji Ezekia alisema kutokuwa na moyo wa kuwajali wengine,kutaka kusikilizwa kila kitu na kutowapa wenzako nafasi ya kuwasikiliza na kujiona ni bora kuliko wao huo pia ni ukatili wa kijinsia.
Mchungaji Revocatus Meza wa Kanisa la Moravian Jimbo la Rukwa ambaye ni Mthiolojia mbobezi na mtaalamu wa masuala ya ukatili.
Post A Comment: