Na Dotto Mwaibale, Singida
KAMISAA wa Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022 Tanzania Bara, Anne Makinda amesema redio zinategemewa sana na wananchi kwa ajili ya kupata taarifa mbalimbali zinazotolewa na Serikali na taasisi zingine zikiwemo za idara ya takwimu.
Makinda ambaye alikuwa mgeni rasmi ameyasema hayo leo Februari 10, 2023 wakati akifungua mafunzo ya wahariri wa habari wa redio jamii yanyayohusu matokeo ya sensa ya watu na makazi ya mwaka 2022 yanayofanyika ukumbi wa mikutano wa ofisi ya mkaguzi mkuu wa hesabu za Serikali mkoani hapa ambayo yatafikia tamati kesho..
Alisema redio jamii pamoja na zile za mikoa zimekuwa redio pendwa kwa wananchi wa mikoa husika kwa kuwa zinatangaza habari nyingi zinazohusu na kugusa maendeleo ya kiuchumi, kijamii.mazingira na utamaduni wa watu na kwa kufanya hivyo zimejiweka karibu na wananchi wa maeneo yao.
“Redio jamii zinaelezwa ni chombo muhimu katika kujenga jamii zenye mwamko, kuwajengea uwezowananchi kuwasilisha mahitaji yao kwa mamlaka husika kwa urahisi na zaidi zinaaminika na jamii” alisema Makinda.
Aidha Makinda alisema wameanza kutoa mafunzo hayo kwa wahariri wa redio na wala sio magazeti na televisheni kwasababu redio ni chombo kinachowafikia wananchi kwa urahisi na katika njia rafiki wakati wote tofauti na njia nyingine za upashanaji habari kama vile magazeti na televisheni, hivi sasa Tanzania Bara kila mkoa una vituo vya redio kati ya viwili hadi vitano ukiachia mikoa kama Dar es Salaam, Dodoma, Mbeya, Morogoro na Mwanza ambayo ina utitiri wa vituo hivyo.
Alisema sababu kuu ya kuanza mafunzo haya kwa redio ni kutokana na uwezo wa redio kuwafikia wananchi katika maeneo yote ya nchi kama ilivyo katika nchi nyingi zinazoendelea kama Tanzania, redio ndio chombo kikuu kinachotegemewa na wananchi wengi kupata habari na kuwa hapa nchini hivi sasa, redio zimejipambanua kwa kuwa na vituo vya redio zaidi ya 200.
Aidha, Makinda alisema kutokana na maendeleo ya teknolojia, siku hizi huhitaji tena kuwa na redio ili uweze kupata matangazo ya redio bali yamerahisishwa hadi mwananchi anaweza kupata matangazo ya redio kiganjani yaani kupitia simu ya mkononi ikiwemo simu za bei nafuu maarufu humu nchini kama Vitochi au kiswaswadu.
“ Matangazo ya redio yanapatikana pia kwa njia ya mtandao yaani intaneti. Katika hali hiyo, nidhahiri kuwa redio ndio chombo pekee ambacho watanzania wengi wanakitegemea kupata taarifa. Mathalan, hata tafiti ambazo tulizifanya wakati wa kupima uwelewa wa wananchi kuhusu Sensa, asilimia 49.0 walisema wamepata taarifa za Sensa kupitia redio ikifuatiwa na asilimia 47kupitia ujumbe mfupi kupitia simu za kiganjani. Hivyo, mafunzo haya kwetu ni muhimu sana kwa kuwa tuna uhakika kuwa yakifanikiwa wananchi wetu wataweza kupata matokeo ya Sensa kwa urahisi zaidi na kusaidia utekelezaji wa mpango kazi wa usambazaji wa mafunzo ya matokeo ya Sensa” alisema Makinda.
Akizungumza kwa niaba ya Mtakwimu Mkuu wa Serikali, Dkt. Albina Chuwa, Mratibu wa Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022, Mkoa wa Singida, Naing'oya Kipuyo, alisema lengo la mafunzo hayo ni kuviwezesha vyombo vya habari kuwa na uelewa mpana wa Matokeo ya Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2022 ili viweze kutimiza wajibu wao wa kusambaza, kuelimisha na kuhamasisha wananchi kutumia matokeo ya Sensa na vikifanya hivyo, vitakuwa vimetimiza wajibu wao kwa taifa hususan kufanikisha malengo ya sensa.
“ NBS imekuwa ikiandaa mafunzo ya aina hii kwa vyombo vya habari mara kwa mara kwa kuwa jukumu letu la uzalishaji na usambazaji takwimu linakuwa rahisi kama tutakuwa na ushirikiano mzuri na wa karibu na vyombo hivi” alisema Kipuyo.
Aidha, Kipuyo alisema kwa kawaida kabla ofisi yao haijafanya mazoezi makubwa ya ukusanyaji takwimu ikiwemo Sensa ya Watu na Makazi wana utaratibu wa kuvifanyia mafunzo maalum vyombo vya habarikuwawezesha kuwa na ufahamu mpana wa tafiti ili viweze kuielewesha jamii kuhusu mazoezi hayo na inafanya hivyo hivyo, hata baada ya matokeo kutolewa ili kuwaelewesha nini kimejiri katika tafiti hizo kwa kuwafundisha na kuwafafanulia matokeo hayo kwa kina iliviweze kuyasambaza kwa wadau wote ipaswavyo.
Alisema katika mnasaba huo, NBS imejenga uhusiano na ushirikiano wa karibu na vyombo vya habari nchini na kama ilivyo kuwa wakati wa Sensa kwani havikuwaangusha kabisavilifanya kazi nzuri na matokeo yake yameonekana.
“Vyombo vya habari ni sehemu ya mafanikio tuliyoyapata katika utekelezaji wa Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2022 ambayo ilikuwa ya kihistoria. Hivyo, sina shaka yoyote kuwa vyombo vya habari vitaendelea na mwenendo ule ule wa kuzipa umuhimu habari za Sensa ambapo kwa sasa ni matokeo ambayo yanapaswa kuwafikia wananchi popote walipo hivyo naomba nichukue fursa hii kuvishukuru kwa dhati” alisema Kipuyo.
Mratibu wa Mtandao wa Redio za Kijamii nchini (TADIO) Cosmas Lupoja alisema mtandao huo umekuwa ukifanya kazi kwa karibu na Serikali na taasisi mbalimbali na kuwa unajumuisha redio wanachama 42 Zanzibar zikiwa tano 5na Tanzania Bara 37.
“Wanachama wetu wengine ni Chama cha Waandishi wa Habari Pemba (Pemba Press Club) Dodoma TV na Dodoma FM ambapo kwa ujumla tuna kuwa 44” alisema Lupoja.
Lupoja alitumia nafasi hiyo kuwashukuru sana Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) kwa ushirikiano mkubwa wanao wapa kwa kuwashirikisha kuanzia mwanzo wa mchakato wa Sensa ya Watu na Makazi 2022 hadi mwisho wake na kueleza kuwa redio za kijamii zimekuwa na mchango mkubwa kutokana na kuwafikia watu wengi zaidi ambapo aliomba ushirikiano huo uendelee kudumu.
Post A Comment: