Na Denis Chambi, Tanga.
Mtanange mkali unaosubiriwa kwa hamu kubwa utashuhudiwa jumamosi hii kwenye uwanja wa shule ya sekondari Popatlal kati ya Madiwani wakiminyana na wakuu wa idara na vitengo wa halmashauri ya jiji la Tanga wakishiriki michuano ya Bonanza watumishi lililoandaliwa na halmashauri hiyo kwa lengo la kumasisha ushiriki wa michezo kwa watumishi wote kuimarisha mahusiano baina yao pamoja na kupambana na magonjwa yasiyoambukiza ikiwemo kisukari.
Michezo mingine itakuwa ni kati ya walimu wa shule za msingi na sekondari ,watumishi waliopo ofisi kuu za halmashauri wakipepetana na wale walipo kwenye vituo vyote vya afya, watendaji wa kata wakitifuana na watendaji wa mitaa ushindani huu ukishirikisha michezo yote ambayo itakuwepo kwa upande wa wanawake na wanaume.
Akizungumza kuelekea bonanza hilo mstahiki meya wa jiji la Tanga Abdulrahman Shillow alisema kuwa ilikuwa ni dhamira ya halmashauri hiyo kuhuisha michezo kuhakikisha kuwa kila mtumishi anashiriki hii ikiwa ni njia moja wapo ya kuepukana na magonjwa yasiyoambukiza ikiwemo kisukari, kuimarisha umoja na mahusiano baina ya watumishi viongozi na wananchi kwa kupitia idara ya michezo kila mwaka kuhakikisha wanashiriki kwa pamoja michezo mbalimbali.
"Halmashauri ya jiji la Tanga tumeamua kwa makusudi na kwa dhamira ya dhati kabisa kuhuisha michezo katika jiji letu kwa maslahi mapana ya wananchi ili kujaribu kuepuka maradhi yasiyoambukiza mfano kisukari maradhi ya moyo sasa tunataka tutengeneze utaratibu wa watu kupenda kufanya mazoezi"
"Tuna vikundi vingi vya mazoezi katika jiji letu la Tanga lakini tumeona kwamba na sisi halmashauri tuzidi kusukuma ufanyaji wa mazoezi kupitia kitengo chetu cha michezo angalau kila mwaka mara moja tuwe na bonanza ambalo litashirikisha watumishi , madiwani na kila ambaye atapenda kushiriki na kuwavutia wengine pia wajisikie kupenda michezo mbalimbali" alisema Shillow.
Akizungumza afisa michezo wa halmashauri ya jiji la Tanga Michael Njaule alibainisha kuwa washindi wa michezo yote watafanikiwa kuondoka na makombe na kuvishwa medal ambayo watadumu nayo kwa muda wa wiki mbili kisha kuyarudisha ofisini huku akiwataka kufanya maandalizi ya mazoezi kwa washiriki wote ili kuweza kuleta ushindani na burudani kama ilivyotarajiwa siku hiyo.
"Mechi kabambe ambayo itakuwepo ni kati ha waheshimiwa madiwani wakiongozwa na mstahiki meya watacheza na wakuu wa idara na vitengo, bonanza letu ni la siku moja mechi zitakuwa ni za mtoano mshindi wa kwanza atapata kombe na medali na kombe watakaa nalo kwa muda wa wiki mbili na nusu kisha litarudi ofisini kwaajili ya kugombaniwa tena msimu ujao na mtu akilichukuwa misimu mitatu mfululizo litakuwa kombe lake" alisema Njaule.
Bonanza ambalo litaanza kwa vikundi mbalimbali vya Jogging kufanya mazoezj ya kukimbia na matembezi na linatarajiwa kufanyika kila mwaka ambapo litaihusisha michezo ya mpira wa miguu, pete , bao, kukimbiza kuku, riadha , mpira wa mikono, kukimbia na magunia, mashindano ya kucheka na hatimaye zawadi mabalimbali kutolewa kwa washindi wa kila mchezo.
Post A Comment: