Na, Elizabeth Paulo; Dodoma

Wito umetolewa kwa wafanyabiashara ambao ni (MADALALI) kuacha kuwarubuni wakulima kwa kuwafuata mashambani na kuwarubuni kwa manufaa binafsi kwani mara baada ya wakulima hao kujua kuwa serikali ina Maghala mazuri watakua na wakati mgumu sana katika utendaji wao wa kazi.

Mkurugenzi Mtendaji Bodi ya Usimamizi Wa Stakabadhi Za Ghala (WRRB) Asangye Bangu ameyasema hayo leo jijini Dodoma alipokua akieleza utekelezaji wa Bodi mbele ya waandishi wa Habari.

 Bangu amesema kumekuwa na wimbi la watu wanaokwenda mashambani kwa wakulima na kuwadalalia mazao na kununua kwa bei ya chini kitu ambacho kinaendelea kudidimiza maendeleo ya wakulima.

"Madalali tunawapenda lakini Natoa wito waache kuwarubuni wakulima wawaache wajiunge katika Mfumo wa Stakabadhi ghalani ili waweze kuuza mazao yao kwa bei ya ushindani iliyopo sokoni kwa kuendelea kuuza mazao shambani inaendelea kuwadidimiza wakulima kwa sababu madalali wengi wananunua mazao kwa bei ya chini tofauti kabisa na bei iliyopo kwenye mfumo,"alitoa wito Bangu

Bangu amesema mafanikio yaliyopatikana baada ya kuanzishwa kwa Mfumo wa Stakabadhi za Ghalamni pamoja na ongezeko la bei za mazao, mapato ya mkulima na mapato ya Serikali kwa wastani wa asilimia 200% kutokana na urasimishaji, ongezeko la uzalishaji wa mazao kwa wastani wa asilimia 12% kwa mwaka,kichecheo cha ubora wa mazao yanayofikishwa sokoni,

Akitaja mafanikio mengine amesema ni pamoja na patikanaji wa takwimu sahihi za mazao yanayopita kwenye Mfumo wa Stakabadhi za Ghala, ongezeko la mapato ya uhakika kwa Serikali Kuu na Serikali Mitaa na kukuza huduma za fedha vijijini,kufanikisha uanzishaji wa Soko la Bidhaa Tanzania.

Mkurugenzi huyo amesema kuwa tangu kuanzishwa kwa Mfumo 2007/08 hadi 2020/21 ukuaji wa uzalishaji umekuwa ukiongezeka kwa wastani wa 12% kwa mwaka ikilinganishwa na ukuaji wa 2% kwa mwaka kabla ya kuanzishwa kwa Mfumo wa Stakabadhi za Ghala.

Sambamba na hilo amesema kuwa tangu mwaka 2007 hadi sasa kilo bilioni 2.3 za mazao ya nafaka zimepitishwa na bodi hiyo na kilo hizo zinatokama na mazao 11 yanayolimwa hapa nchini.

"Kwa mfano katika zao la Korosho mara baada ya kuanzishwa kwa Mfumo palikuwa na ongezeko la asilimia 164% la bei kutoka Ths 350.00 msimu wa 2006/07 hadi kufikia Tsh 925.00 msimu wa 2007/08 mwaka wa kuanza wa Mfumo; katika miaka minane tokea kuanzishwa kwa Mfumo 2007/08 hadi 2014/15 wastani wa ongezeko la bei kwa mwaka ulikuwa 25% kulinganisha na ongezeko la bei miaka minane kabla ya kuanzishwa kwa Mfumo la 12% kwa mwaka kaunzia mwaka 1998/99 hadi 2006/07," amebainisha Bangu

Aidha, Bodi imeendelea na juhudi za kuboresha Mfumo uliokuwepo wa kizamani wa Usimamizi wa ghala, ambapo kushirikiana na Bodi ya TEHAMA inakuja na Mfumo mpya wenye kuweza kurahisisha kazi za maandalizi ya taarifa, utoaji stakabadhi na udhibiti wa matukio ghalani hivyo kupunguza muda wa michakato na kuongeza ufanisi na usalama wa mzigo.

"Majaribio ya Mfumo wa Maombi ya Leseni Mtandaoni yamefanyika na mapendekezo ya maboresho yamepelekwa kwa programmers kwa ajili ya kufanyiwa kazi,"amesema Bangu

Hata hivyo Bangu amesema kuwa bodi inashirikiana na taasisi mbalimbali kwa ajili ya kutoa elimu kwa wakulima kwa lengo la kuwafanya wakulima kupata mazao bora na salama ambayo yataweza kuingia katika soko la ndani na nje ya nchi.

Aidha ameeleza kuwa bodi hiyo kwa sasa imekuwa ikishiriki kupata mazao ambayo hayapo katika bodi ili nayo yaweze kuingizwa katika ghala huku wakiangalia ni jinsi gani ya kuanzisha maghala ya mazao ya kuoza kama vile maparachichi na nyanya pamoja na mazao mengine.

Ukiachana na mazao hayo ameeleza kuwa kwa sasa bodi inafikiria na ipo katika mazungumzo na wizara ya mifugo ili kuweza kuanzisha maghala ya mifugo kama vile ngozi sambamba na mazao ya nyuki .

Hata hivyo amezitaja changamoto kadhaa kuwa ni pamoja na kukosekana kwa elimu juu ya mfumo ambao unatumiwa na bodi hiyo na kusababisha kuwepo na maneno ya uzushi juu ya mfumo.

Bodi ya Usimamizi wa Stakabadhi za Ghala (WRRB) ni taasisi iliyofanikiwa chini ya Wizara ya Viwanda na Biashara iliyoundwa kwa Sheria Namba 10 ya 2005 na Marekebisho Kifungu 4 Sura 339 R.E. 2016 iliyopewa majukumu chini ya Kifungu 5 (a-j) ikiwemo kutoa leseni kwa waendesha ghala, meneja dhamana na wagakuzi wa ghala; kuchapa and kuidhinisha vitabu vya Stakabadhi za Ghala, kusajili na kuingiza taarifa za wadau muhimu wa mfumo, kuwakilisha nchi katika masuala ya taifa na kimataifa yahusuyo Mfumo wa Stakabadhi za Ghala pamoja na majukumu mengine kama taasisi itakavyoelekezwa na Mhe. Waziri wa Viwanda na Biashara.

Share To:

ELIZA DOM

Post A Comment: