Na; Elizabeth Paulo, Dodoma 

Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Iringa (IRUWASA) imevuka lengo la sera ya maji na ilani ya Chama Cha Mapinduzi ya kutaka kufikia asilimia 95 kutoa huduma ya usambazaji Maji huku Mamlaka ikivuka lengo hilo kwa kufikisha asilimia 97 na muda wa upatikanaji wa maji ukiwa wastani wa saa 23 kwa siku.


Kwa Mujibu wa tafiti za Mamlaka ya Udhibiti wa huduma za nishati na Maji (EWURA) katika kipindi cha miaka mitatu IRUWASA imekua nafasi ya tatu kwa kutoa huduma bora za maji na kusimamia vizuri fedha zinazoelekezwa na Serikali katika kutekeleza miradi mbalimbali ya maji Iringa.


Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Iringa (IRUWASA) Mhandisi David Pallangyo, Amebainisha hayo leo Jijini Dodoma alipokutana na waandishi wa Habari wakati akieleza utekelezaji wa majukumu ya Mamlaka hiyo.


"Idadi ya wateja/Maunganisho ya Majisafi imeongezeka kutoka elfu 28,133 mwaka 2020 hadi elfu 40, 549 kwa mwaka 2022".Alisema Pallangyo


Katika kipindi cha mwaka 2021, Serikali iliipatia IRUWASA kiasi cha Shilingi 1,025,539,313 zilizotumika kutekeleza miradi miwili yenye lengo la kuboresha huduma za maji katika maeneo ya Manispaa ya Iringa na Mji wa Ilula. 

"Miradi hii imetekelezwa chini ya Mpango wa Maendeleo ya Ustawi wa Taifa na Mapambano dhidi ya UVIKO -19 na imekamilika kwa asilimia 100 ikinufaisha jumla ya watu 15,398, kadhalika mradi wa maji wa Isimani Kilolo ulianza kutekelezwa Aprili, 2020 kwa njia ya force account kwa makadirio ya gharama ya Shilingi 9,270,306,365". Alisema 



Hadi mwezi Desemba, 2022, mradi wa Isimani-Kilolo ulikuwa umetekelezwa kwa asilimia 82 na jumla ya vijiji 20 kati ya 29 vinapata maji kwa sasa. Mradi unatarajiwa kukamilika mwezi Aprili, 2023. Aidha, kati ya Shilingi 9,270,306,365, IRUWASA imeshapokea kiasi cha Shilingi bilioni 7.8 sawa na asilimia 84 ya gharama zote. 


 

"Mradi huu utakapokamilika, utaongeza uzalishaji wa maji kutoka lita 2,238,000 kwa siku hadi lita 4,656,000 kwa siku na hivyo kukidhi mahitaji kwa asilimia 100 na Wananchi watapata huduma ya maji kwa umbali usiozidi mita 400 na kila kituo kitahudumia wananchi wasiozidi 250 na wengine watapata huduma majumbani". Alisema Pallangyo 


Katika kuhakikisha wananchi wanaondokana na adha ya upatikanaji wa huduma za maji Serikali imepanga kutekeleza mradi kupitia mkopo wenye masharti nafuu kutoka Serikali ya Korea wenye thamani ya Dola za Marekani milioni 88.4 na utekelezaji unatarajiwa kuanza mwezi Mei 2023. Aidha, ujenzi unatarajiwa kuanza mwezi Aprili 2024 na kukamilika mwaka 2027 ambapo watanzania takribani 6400 wanatarajiwa kupata ajira za mkataba




Katika eneo la TEHAMA, IRUWASA imefanikiwa kwa kufunga mita za malipo kabla kwa wateja 6,752 na kuwa Mamlaka inayoongoza nchini kwa kufunga mita nyingi za maji za malipo kabla ambapo tangu mwezi Machi, 2016 Mamlaka ilianza kuzifungia mita za malipo ya kabla Taasisi za Serikali na wateja wa kawaida na wafanyabiashara ili kudhibiti ongezeko la madeni.


Chanzo kikuu cha uzalishaji maji kwa Manispaa ya Iringa na maeneo ya pembezoni ni Mto Ruaha Mdogo na vyanzo vingine vidogo ni pamoja na chemichemi ya Kitwiru na visima vya viwili virefu vya Nyamhanga na Mawelewele.


Maji yanayozalishwa na IRUWASA kutoka kwenye vyanzo vilivyotajwa, husafishwa na kutibiwa hadi kukidhi viwango vya ubora wa maji vya Tanzania kabla ya kusambazwa kwa wateja.







Share To:

ELIZA DOM

Post A Comment: