Na. Angela Msimbira OR-TAMISEMI
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe. Angellah Kairuki ameagiza Chuo cha Serikali za Mitaa Hombolo kuhakikisha wanaweka utaratibu wa kufanya utafiti wa masomo wanayotoa kama yanatoa tija kwa wanafunzi na kuwawezesha kutimiza majukumu yao wanapoajiriwa.
Mhe. Kairuki ameyasema hayo leo tarehe 17 Februari, 2023 Jijini Dodoma wakati alipotembelea chuo hicho ikiwa ni utaratibu aliojipangia wa kutembelea taasisi zilizoko chini ya Ofisi ya Rais-TAMISEMI kwa lengo kujionea utekelezaji wa majukumu ya taasisi hizo.
Waziri Kairuki ameendelea kufafanua kuwa chuo hicho kina jukumu la kufanya tafiti za kina kujua wanafunzi wanaomaliza masomo yao wanauwezo wa kutekeleza majukumu yao ipasavyo na kuongeza tija katika Halmashauri ili kujiridhisha kuwa mafunzo yanayotolewa yanatija na kuwawezesha kutimiza lile lililokusudiwa na Serikali.
Amesema kuwa chuo kina jukumu kubwa la kuangalia malengo ya uanzishwaji wake kwa kuzingatia kuwa Mamlaka za Serikali za Mitaa zinajukumu kufanya kazi kikatiba, kisheria kutokana na majukumu hivyo Chuo cha Serikali za Mitaa Hombolo kina jukumu la kuhakikisha wanawajengea uwezo na weledi wanafunzi hao ili waweze kwenda kuwatumikia wananchi katika Halmashauri hivyo ni muhimu kuangalia kama wanauwezo wa kufanya kazi.
“Wanafunzi wengi wanaomaliza katika chuo cha Serikali za Mitaa Hombolo wanategemewa sana kufanya kazi katika Mamlaka za Serikali za Mitaa, hivyo ni jukumu letu kuhakikisha kuwa mafunzo yanayotolewa yanaenda sambamba na matakwa ya Serikali,tuwajengee uwezo, uadilifu na uaminifu katika kutekeleza majukumu yao” amesema Waziri Kairuki
Amesema kuwa Serikali inategemea kuwa na idadi kubwa ya wanafunzi wanaosoma katika chuo cha Serikali za Mitaa Hombolo wanategemewa kwenda kufanya kazi katika Mamlaka za Serikali za Mitaa hivyo amewataka kuweka mikakati ya kuhakikisha tunawajengea uwezo na mbinu za kutimiza majukumu yao
Naye Mwenyekiti wa Bodi Prof. Joseph amesema chuo hicho kipo katika mkakati wa kutekeleza mpango wa maendeleo kwa kuboresha miundombinu ya kufundishia na ujifunzaji kwa lengo la kuboresha mazingira ya chuo na pia kinaendelea kuwajengea uwezo wafanyakazi kwa kuwasomesha katika ngazi mbalimbali pamoja shahada za uzamivu,umahiri na shahada za awali.
Amesema chuo kimeweza kuboresha mifumo ya TEHAMA na mifumo ya uendeshaji hasa ya kudahili wanafunzi na mifumo ya ukusanyaji wa mapato nia ikiwa ni kuwezesha menejimenti kuweza kusimamia rasilimali zilizopo.
Aidha, amesema chuo kipo katika mkakati wa kuhuisha mitaala ya chuo ili masomo yanayotolewa yaendane na mahitaji ya soko na kutengeneza programu mpya kwa kuangalia mahitaji.
Post A Comment: