Naibu Waziri Ofisi ya Rais – TAMISEMI, Dkt. Festo J. Dugange(Mb) amezitaka Halmashauri kuhakikisha zinakusanya Mapato ya ndani kwa ufanisi ili kuondokana na utegemezi wa kila fedha za miradi ya maendeleo kutoka Serikali kuu.
Ameeleza hayo leo tarehe 21 Februari 2023 wakati akiongea na Watumishi wa Halmashauri ya Kiteto mara baada ya kuwasili wilaya hapo katika mwendelezo wa ziara ya kikazi Mkoani Manyara.
“Tudhibiti minaya ya upotevu wa mapato kwa kutumia mashine za POS kikamilifu, pamoja na kubuni vyanzo vipya vya mapato ya ndani” amesema Dkt. Dugange
Dkt. Dugange amesema kumekuwa na tabia katika baadhi ya Watumishi katika halmashauri kuzima mashine za POS na kutumia nafasi hiyo kuiba fedha za mapato ya halmashauri jambo ambalo halikubaliki.
Amezitaka halmashauri kuelekeza asilimia 40 ya Mapato ya halmashauri kwenye miradi ya maendeleo yenye tija na kutatua changamoto za Wananchi ikiwa ni pamoja kukamilisha miradi ambayo haijakamilishwa kwa muda mrefu.
Aidha, Dkt. Dugange ameelekeza mikopo ya asilimia 10 kwa ajili ya Vikundi ya Wanawake, Walemavu na Vijana itolelewe kwa kufuata taratibu ili kuviwezeha vikundi hivyo kunufaika ili viwezee kurejesha mikopo hiyo.
Dkt. Dugange ameipongeza Halmashauri ya wilaya Kiteto kwa kukusanya bilioni 1.69 kufikia tarehe 20/02/2023 sawa na asilimia 68 ya lengo la mwaka wa fedha 2022/23.
Kadhalika, Dkt. Dugange amewataka Watumishi wa halmashauri kutekeleza kikamilifu majukumu yao kwa Weledi na kujitathimini wenyewe utendaji kazi wao na kuhakikisha wanatatua kero za wananchi.
Post A Comment: