OR TAMISEMI - Manyara
Naibu Waziri Ofisi ya Rais – TAMISEMI, Dkt. Festo J. Dugange(Mb) amebaini mianya ya upotevu wa madawa katika hospitali ya wilaya Babati na ametoa siku saba timu maalum kufanya uchunguzi wa mfumo wa uagizaji, Utunzaji na Utoaji wa dawa katika hospitali hiyo.
Amebaini hayo leo tarehe 20 Februari wakati akikagua utoaji wa huduma katika hospitali ya wilaya ya Babati wakati wa ziara yake ya kikazi Mkoa wa Manyara.
“Sijaridhishwa na utunzaji wa takwimu za uagizaji, Utunzaji na Utoaji wa dawa kwa wagonjwa, vilevile hakuna dawa kwa kiwango kinachotakiwa kwenye bohari ya dawa ktk hospitali hii” amesema Dkt. Dugange
Amesema Serikali imeweka utaratibu wa kuagiza madawa, kupokea, kutunza na kutoa dawa kwa wagonjwa lakini taratibu hizo hazifuatwi jambo ambalo linatoa mianya ya wizi wa dawa katika hospitali hiyo.
Dkt. Dugange amemuagiza Katibu Tawala wa Mkoa Manyara ndani ya siku saba kuhakikisha analeta timu maalum ya kufanya uchunguzi wa Uagizaji, Utunzaji na Utoaji wa dawa ili hatua stahiki zichukuliwe iwapo itajiridhisha upotevu wa madawa.
Aidha, Dkt. Dugange amebaini uzembe mkubwa katika usimamizi wa ujenzi wa Wodi tatu na jengo la kuhifadhi Maiti ambapo Serikali ilileta shilingi milioni 750 lakini ipo kwenye akaunti zaidi ya miezi mitatu na hakuna kazi iliyofanyika na ameagiza ifikapo tarehe 30 Mei 2023 ujenzi wodi hizo uwe umekamilika.
Kadhalika, Amemuagiza Mganga mkuu wa wilaya kuhakikisha Jengo la upasuaji na Wodi ya Wazazi ambavyo vipo katika hatua za ukamilishaji, kuhakikisha vinakamilika na kuanza kutoa huduma ifikapo tarehe 15/03/ 2023.
Dkt. Dugange amemuagiza Meneja wa TARURA wilaya ya Babati kufanya upembuzi yakinifu wa barabara inayokwenda katika hospitali ya wilaya ili iweze kutengewa bajeti na kutengenezwa.
Post A Comment: