Na John Walter-Babati
Mkuu wa Wilaya ya Babati Lazaro Twange ameagiza watu waliovamia eneo la Msitu wa asili wa kijiji cha Endaw hekari 192 katika kata ya Qameyu Halmashauri ya Wilaya ya Babati mkoani Manyara kuhama haraka na kusitisha Shughuli zote.
Msitu huo  ulianza mwaka 2010.
Twange amesema hawezi kuvumilia kuona uharibifu wa misitu unafanywa na watu wachache halafu wengi wanateseka na matokeo ya uharibifu huo.
Amesema lazima maagizo ya serikali yanayotolewa na makamu wa rais Dr. Philip Mpango kila halmashauri kutunza mazingira na kupanda yazingatiwe katika wilaya ya Babati.
Mkuu wa wilaya amemuagiza mtendaji na mwenyekiti wa kijiji kurejesha fedha za watu wote waliotoa fedha zao ndani ya wiki moja kuanzia leo Februari 17,2023 na warejeshe ardhi kwa kijiji.
Aidha ameagiza afisa mtendaji achukuliwe hatua za kinidhamu kwa kushindwa kutekeleza maagizo yaliyotolewa na Mkurugenzi kwa ajili ya kuwaepusha wananchi kuingia  katika Msitu huo.
Wananchi wamemwambia mkuu wa wilaya kwamba eneo hilo walikabidhiwa na uongozi wa kijiji baada ya kufanyika Mkutano mkuu wa kisheria kwa kutoa shilingi laki mbili na elfu hamsini kwa kila heka moja.
Diwani wa kata ya Qameyu Bernad Fissoo kwa niaba ya wananchi ameomba serikali iangalie namna nyingine ya kuwasaidia kwa ajili ya huduma za kijamii.
Kwa upande wa wakala wa Misitu TFS wilaya ya Babati wamesema kwa kuwa kwenye mpango wao wa uhifadhi wa msitu wa kijiji wa Endaw ni kuhifadhi kwa uhifadhi endelevu na hakuna kipengele kinachoelezea eneo ambalo linapangiwa matumizi mengine, timu imeona kuwa hakuna eneo linalofaa kupangiwa matumizi ya shughuli za jamii bila kuathiri malengo ya uhifadhi.
“Maeneo  mengi ni vyanzo vya maji, hivyo wataalamu waliona isingefaa kufanyika shughuli za kilimo” Alieleza afisa wa TFS.
Kwa upande wa Mwanasheria wa Halamashauri ya wilaya ya Babati Godfrey Jafari amesema Kibali cha kijiji kuruhusiwa kusafisha msitu kwa ajili ya shughuli mbalimbali kilifutwa kutokana na mapungufu yaliyojitokeza.
Wananchi wameeleza kuwa waliuziwa na kijiji  maeneo hayo kwa shilingi 250,000 kwa hekari moja huku wengine wakiyauza kwa watu wengine.
Ikumbukwe serikali imekuwa ikisisitiza Wananchi kupanda miti na kutunza Mazingira pamoja na kila Halmashauri nchini kupanda miti Milioni Moja na laki tano kila mwaka.
Uharibifu wa misiti umekuwa ulichangia kwa kiwango kikubwa mabadiliko ya tabia nchi hivyo kupelekea mvua kuwa za kusuasua.


Share To:

Post A Comment: