Mwenyekiti wa chama cha mapinduzi CCM Mkoa wa Iringa Daud Yassin akiongea wakati wa uapisho wa mkuu wa wilaya ya Mufindi Dkt Linda Salekwa.
Na Fredy Mgunda, Iringa.
CHAMA cha mapinduzi CCM Mkoa wa Iringa kimesema hakitamfumbia macho mtendaji yoyote wa serikali atakayetekeleza miradi chini ya kiwango.
Akizungumza wakati wa uapisho wa mkuu wa wilaya ya Mufindi, mwenyekiti wa chama cha mapinduzi CCM Mkoa wa Iringa Daud Yassin alisema kuwa chama kitaendelea kuisimamia serikali kila Kona ili kuhakikisha wanatekeleza miradi inavyotakiwa.
Yassin alisema kuwa watakuwa wakali kwenye miradi ambayo itakuwa imetekelezwa chini ya kiwango au hailingani na thamani ya fedha ambazo serikali imetoa kwenye mradi husika.
Alisema kuwa wataendelea kusimamia serikali ili kuhakikisha wanatekeleza vilivyo Ilani ya chama cha mapinduzi CCM ya mwaka 2020/2025 kama ambavyo inasema.
Yassin alisema kuwa watahakikisha wanaisimamia serikali kutatua changamoto za wananchi kama ambavyo inatakiwa ili kuwawezesha wananchi kufanya shughuli za kimaendeleo bila kuwa na changamoto zozote zile.
Alisema kuwa chama cha mapinduzi CCM Mkoa wa Iringa kimejipanga kuhakikisha wanashinda uchaguzi wa serikali za mitaa,udiwani,ubunge na urais kwa asilimia 100 hivyo wapinzani hawawezi kupata hata kiti kimoja mkoani Iringa.
Yassin alisema kuwa chama cha mapinduzi CCM Mkoa wa Iringa kinampongeza mkuu wa mkoa wa Iringa Halima Dendego kwa utekelezaji wa Ilani mzuri hivyo jukumu la chama hicho kuhakikisha wanafikisha elimu kila kona ya mkoa wa Iringa.
Aliwataka viongozi wa wilaya kutoa ushirikiano mkubwa kwa viongozi wa chama cha CCM wilaya kama ambayo mkuu wa mkoa wa Iringa Halima Dendego anafanya.
Mwenyekiti wa chama cha mapinduzi CCM Mkoa wa Iringa Daud Yassin alimazia kwa kumpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa anayoifanya ya kuijenga nchi kiuchumi na kutekeleza vizuri Ilani ya CCM ya mwaka 2020/2025.
Post A Comment: