Mwenyekiti wa UVCCM mkoa wa Iringa Agrey Tonga akiongea na vijana juu ya umuhimu wa kuchangia damu salama kwa ajili ya kuokoa maisha ya watu wengine
Baadhi ya vijana wa UVCCM mkoa wa Iringa waliojitokeza kuchangia damu salama kwa ajili ya kuokoa maisha ya watu wengine
Mwanachama wa chama mapinduzi CCM Mkoa wa Iringa akijumuika na UVCCM mkoa wa Iringa kuchangia damu salama kwa ajili ya kuokoa maisha ya watu wengine
Mwenyekiti wa madereva Bajaji Manispaa ya Iringa Melabu Kihwele akijumuika na UVCCM mkoa wa Iringa kuchangia damu salama kwa ajili ya kuokoa maisha ya watu wengine


Na Fredy Mgunda, Iringa.



ZAIDI ya vijana 300 wa umoja wa vijana wa chama cha mapinduzi Mkoa wa Iringa (UVCCM) wamejitokeza kuchangia damu ili kuokoa maisha ya watu ambao wanakuwa na uhitaji wa damu.

Akizungumza wakati wa zoezi la uchangiaji damu katika hospitali ya Rufaa mkoa wa Iringa, mwenyekiti wa UVCCM mkoa wa Iringa Agrey Tonga alisema kuwa watu wengi wamekuwa wanapoteza maisha kutokana na kukosekana kwa huduma ya damu salama.

Tonga aliwataka vijana wa chama hicho na watanzania kwa ujumla kujitokeza kuchangia damu salama kwa ajili kuokoa maisha ya watu wengine wenye uhitaji huduma ya damu salama kuokoa maisha yao.

Alisema kuwa vijana wengi hivi karibuni wamekuwa ndio wahitaji wakubwa wa kupata huduma ya damu salama kutokana ajali nyingi za Bajaji na bodaboda ambazo kwa kiasi kikubwa zinasabishwa na vijana wenyewe.

Tonga alisema kuwa kundi la wanawake na watoto nao wamekuwa na uhitaji mkubwa wa huduma ya damu salama,hasa wanawake kipindi ambacho wanatoka kujifungua.


Mwenyekiti wa UVCCM mkoa wa Iringa Agrey Tonga alimazia kwa kuwaomba watanzania kujitokeza mara kwa mara kuchangia damu katika hospitali mbalimbali ili kuokoa maisha ya watu wengine kutoka na kuendelea kuwa na Upungufu wa damu katika hospitali mbalimbali hapa nchini.


Alisema kuwa katika kuhakikisha idadi ya vifo vya  kina Mama wanaopoteza damu nyingi wakati wa kujifungua vinapungua Ofisi ya Mganga mkuu Mkoa wa Iringa kwa kushirikiana na Umoja wa Vijana wa chama Cha mapinduzi Mkoa wa Iringa (UVCCM) waliratibu zoezi la uchangiaji damu katika hospital ya Mkoa ili kuongeza damu kwa kuwa takribani miezi mitatu sasa hospital ya Rufaa ya mkoani Iringa inakabiliwa na Upungufu wa damu salama.

Kwa upande wake Mratibu damu salama Mkoa wa wa Iringa,Dkt. Hubert Swalo alisema kuwa hospitali ya Rufaa mkoani Iringa inakabiliwa na uhaba wa damu kwa takribani miezi 3 sasa kwa kuwa uhitaji wa damu salama ni zaidi ya Unit 250 kwa mwezi.

Dkt Swalo alisema kuwa wachangiaji wakubwa wa damu ni wanafunzi wa sekondari na vyuo vikuu hivyo kwa kipindi cha likizo hospitali nyingi hukabiliwa na tatizo la Upungufu wa damu salama.

Aliwaomba wananchi wengine kuendelea kujitokeza mara kwa mara kuchangia damu salama kwa ajili ya kuokoa maisha ya ndugu zao na watu wengine maana ukichangia damu hujui itamsaidia nani hapo baadae.


Dkt Swalo alisema kuwa zaidi ya Unit 300 zilipatikana katika zoezi la uchangiaji damu ikiwa ni 100% ya lengo, hali ambayo itaenda kuleta ahueni katika hospitali ya Rufaa Mkoani Iringa huku hamasa kwa makundi mengine ikihitajika kwa kuwa hakuna kiwanda kinachotengeneza Damu.

Nao baadhi ya vijana wa UVCCM mkoa wa Iringa waliojitokeza kuchangia damu walisema kuwa zoezi la uchangiaji wa damu linatakiwa kuwa endelevu kwa wananchi wote ili kuokoa maisha ya watu wenye mahitaji ya damu kuokoa maisha yao.

Walisema kuwa jambo la uchangiaji damu sio jambo la serikali au jambo la kisiasa bali vijana na wananchi wote wanatakiwa kujitokeza kuchangia damu kwa ajili ya kuokoa maisha ya watu wengine.
Share To:

mwangaza wa hbari

Post A Comment: