Waziri wa Habari,Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Nape Nnauye (katikati) akikata utepe kuashia uzinduzi wa Mnara wa Simu wa Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL) uliojengwa na Serikali kwa kushirikiana na Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) katika hafla iliyofanyika jana Kijiji cha Misughaa kilichopo Wilaya ya Ikungi  mkoani Singida.  


Na Dotto Mwaibale, Singida

WAZIRI wa Habari,Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Nape Nnauye amesema kutokana na kasi ya ukuaji wa teknolojia Serikali inafanya kazi kubwa ya kuwekeza kwenye sekta ya mawasiliano kwa kujenga minara ya simu ili kuwawezesha wananchi kupata mawasiliano kote nchini.

Nape ameyasema hayo jana Januari 11, 2022  wakati akizindua mnara wa simu wa Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL) uliojengwa na Serikali kwa kushirikiana na Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) katika Kijiji cha Misughaa kilichopo Wilaya ya Ikungi  mkoani Singida.

Kuzinduliwa kwa mnara huo kuna kwenda kuondoa adha ya muda mrefu waliokuwa wakiipata wananchi wa vijiji sita kutoka Kata za Kikio na Misughaa ya kukosa huduma ya mawasiliano ambapo katika Kata ya Misughaa ni  Kijiji cha Msule, Sakaa na Misughaa na Kata ya Kikio ni Mkunguwakihendo, Munane na Nkundi .

Nape alisema katika Mkoa wa Singida kuna miradi 31 ya ujenzi wa minara, miradi 27 ikiwa imekwisha kamilika huku minne kati ya hiyo ikiendelea na yote ikiwa na thamani ya Sh.5 Bilioni na kuwa maeneo mengine itakapo jengwa minara hiyo ni Kata ya Mang’onyi na Makiungu,kama alivyoomba Mbunge wa jimbo hilo Miraji Mtaturu.

Alisema Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutambua changamoto hiyo ametoa kiasi hicho cha fedha na kuwa kuna miradi zaidi 33 imekwisha tangazwa na tenda yake itafunguliwa mwishoni mwa mwezi huu kwa ajili ya kuongeza minara mingi zaidi.

Nape aliomba inapojengwa minara hiyo kuwepo na miundombinu wezeshi kama umeme na barabara ili kupunguza gharama za kuiendesha.

Katika hatua nyingine Nape aliahidi kutoa saruji mifuko 400 kwa ajili ya Shule ya Sekondari ya Dk.Shein saruji ambayo ataipata kwa kushirikiana na makampuni ya simu mbalimbali na kabla ya kutaoa ahadi hiyo wazee wa kijiji hicho walimpa heshima ya uchifu kwa kumpa ngao, mkuki na kuvikwa mgolole.

Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL) Mhandisi Peter Ulanga alisema ujenzi wa mnara huo ulikamilika tangu mwaka jana na kazi iliyobakia ni ujenzi wa nyumba ya mlinzi na choo na kuwa mnara huo unafanya kazi vizuri na huduma kwa wananchi inapatikana.

Mkuu wa Mkoa wa Singida alimwakikishia Waziri Nape kuwa umeme na miundombinu ya barabara itafikishwa kwenye eneo hilo la mnara na kuwa kilichofanyika kinakwenda sanjari na mageuzi manne ya teknolojia na akaomba uwekezaji zaidi uwe kwenye mawasiliano na akatoa ombi kwa TTCL kuruhusu makampuni mengine kwenda kufunga mitambo yao kwenye eneo hilo pamoja na kushusha bei ya upangaji.

Mtendaji Mkuu wa Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) Justina Mashiba alisema  walitoa Sh. 160 Milioni kwa ajili ya kujenga mnara huo na kuongeza kuwa kila alipokuwa akikutana na Mbunge wa Jimbo la Singida Mashariki Miraji Mtaturu alikuwa akisistiza kupata mnara huo kwa ajili ya wananchi wa Misughaa.

Mkuu wa Wilaya ya Ikungi Jerry Muro alisema mnara huo utasaidia sana katika kuimarisha suala zima la ulizi na usalama na kukuza uchumi wa eneo hilo kwani wananchi wataweza kufungua vibanda kwa M-Pesa na kujiongezea kipata tofauti na kabla ya hapo ambapo walikuwa wakisafiri kwenda Kata za Makiungu na Kikio kufuata huduma hiyo.

Mbunge wa Jimbo la Singida Mashariki Miraji Mtaturu aliishukuru Serikali chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kujenga mnara huo ambapo tangu nchi hii ipate uhuru wananchi wa eneo hilo la Bonde la Ufa walikuwa hawajawahi kuwa na mawasiliano.

“Serikali inafanya kazi kubwa katika sekta mbalimbali kuanzia ya afya, elimu, barabarao na  mawasiliano hakika kila mpenda maendeleo anapaswa kumuunga mkono Rais wetu na serikali yake kwa kazi hii kubwa inayofanyika” alisema Mtaturu.

Alisema mnara  huo una kwenda kuongeza ufaulu kwa Wanafunzi wa Shule ya Sekondari Dk.Shein kwani watatumia intaneti kujifunza mambo mbalimbali yahusuo masomo pamoja na kukuza uchumi wa wananchi wa eneo hilo.

Mtaturu alitoa sola tatu, vifaa vya kuunganishia umeme kama nyaya na vingine kwa ajili ya kusaidia umeme kufungwa kwenye shule hiyo.

Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL) Mhandisi Peter Ulanga (kushoto) akitoa taarifa ya ujenzi wa mnara huo mbele ya Waziri wa Habari,Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Nape Nnauye.

Mkuu wa Mkoa wa Singida, Peter Serukamba, akizungumza kwenye uzinduzi huo.

Mkuu wa Wilaya ya Ikungi Jerry Muro akizungumza kwenye uzinduzi huo.

Mtendaji Mkuu wa Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) Justina Mashiba, akizungumzia mradi huo.

Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Nape Nnauye (katikati) Mbunge wa Jimbo la Singida Mashariki, Miraji Mtaturu (kushoto) na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi, Justice Kijazi wakiserebuka sanjari na wakina mama wa Kijiji cha Misughaa kabla ya uzinduzi wa mnara huo.

Mbunge wa Jimbo la Singida Mashariki, Miraji Mtaturu akielezea kwa kifupi mradi huo na kutoa shukurani kwa niaba ya wananchi kwa  Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwezesha fedha za ujenzi wa mnara huo.

Meneja wa TTCL Mkoa wa Singida, Agustino Mwakyembe akizungumza kwenye uzinduzi huo.

Muonekano wamnara huo.
Viongozi na wananchi wakiwa kwenye hafla hiyo.
Wanafunzi wa Shule ya Dk. Shein wakiwa kwenye hafla hiyo.
Hafla ikiendelea.
Katibu Tawala wa Wilaya ya Ikungi, Winfrida Funto, akizungumza kwenye hafla hiyo.
Wanafunzi wakiwa kwenye hafla hiyo.
Hafla ikiendelea.
Waziri wa Habari,Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Nape Nnauye, akionesha furaha yake baada ya Wazee wa Kijiji cha Misughaa kumpa heshima ya uchifu kwa kumvika mgolole na kumpa ngao na mkuki ikiwa ni heshima ya kimila kwa kabila la Wanyaturu. Kulia ni Mbunge wa Jimbola Singida Mashariki Miraji Mtaturu akifurahia tukio hilo.
Share To:

dotto mwaibale

Post A Comment: