WATU watatu wamefariki dunia akiwemo raia wa Kenya baada ya magari kugongana uso kwa uso na kuteketea kwa moto katika eneo la Maili Kumi wilayani Handeni, Tanga.
Akizungumza na waandishi wa habari, Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa Tanga, ACP David Chidingi, amesema kuwa ajali hiyo ilitokea saa saba usiku wa Januari 6, 2023.
Amesema ajali hiyo imehusisha gari aina ya fuso lenye namba za usajili T 800 CUT, likiwa limebeba mbogamboga likitokea Moshi, Kilimanjaro kuelekea Dar es Salaam, kugongana na gari aina ya Scania lililokuwa limebeba gesi lenye namba za usajili KCH 044T lenye tela namba ZF 9606 ambalo lilikuwa linatoka Dar es Salaam kuelekea Kenya.
Aliwataja marehemu kuwa ni raia wa Kenya Edward Njoroge aliyekuwa akiendesha Scania pamoja na dereva wa Fuso Goodlove Lema na abiria aliyekuwa kwenye fuso ambaye jina lake halikuweza kutambulika.
Majeruhi Maggid Juma amekimbizwa hospitali ya Magunga kwa matibabu zaidi, huku miili ya marehemu ikiwa imehifadhiwa hospitali.
Amesema chanzo cha ajali hiyo ni uzembe wa dereva wa Fuso kutaka kulipita gari la mbele yake bila kuchukuwa tahadhari.
Post A Comment: