Daktari Faraja Liyamuya kutoka wizara ya afya katika mpango wa taifa wa kudhibiti magonjwa ambayo hayapewi kipaumbele akizungumza na waandishi wa habari jijini Tanga katika kituo cha afya Mwakidila walipoweka kambi ya siku tano kwaajili ya kutoa huduma ya upasuaji kwa wagonjwa wa Ngiri maji .
Mganga mkuu wa mkoa wa Tanga Japhet Simeo akizungumza na waandishi wa habari katika kituo cha afya Mwakidila jijini Tanga kuhusu kampeni ya kitaifa ya kutoa huduma kwa wagonjwa wa magonjwa yasiyopewa kipaumbele ikiwemo Ngirimaji
Na Denis Chambi, Tanga.
Tafiti zilizofanywa na wizara ya afya juu ya magonjwa yasiyopewa kipaumbele yakiwemo Ngirimaji na Matende zimebaini kuwa jumla ya halmashauri 119 hapa nchini kati ya 184 zina waathirika wengi wa magonjwa hayo huku jamii ikitajwa kutokuwa na uelewa wa kutosha juu ya sababu zinazopelekea kuongezeka kwa wagonjwa mbalimbali wengi wakiyahusisha na imani potofu.
Katika kuhakikisha kuwa magonjwa hayo yanapungua na kuyatokomezwa kabisa serikali imekuja na mikakati kabambe ya kutoa matibabu bure kwa wahanga ikiwemo upasuaji wa ngiri maji kote nchini mpango unaofadhiliwa na And Fund kutoka Uingereza ukiwa bado unaendelea kila mkoa hapa nchini unakilenga pia kuwafikia wagonjwa wengine elfu kumi.
Akizungumza mkoani Tanga walikoweka kambi ya siku tano kutoa huduma za upasuaji wa ngiri maji pamoja na dawa Daktari Faraja Liyamuya kutoka wizara ya afya katika mpango wa taifa wa kudhibiti magonjwa ambayo hayapewi kipaumbele amesema kuwa kufwatia tafiti zilizofanyika katika halmashauri zote 184 zilibaini kuwa kati ya hizo ni halmashauri 119 ndizo zina maambukizi na vimelea vingi vya magonjwa hayo ikiwemo Ngiri maji na matende.
Amesema kuwa kumekuwa na nadharia tofauti tofauti zilizokuwa zimejengeka kwenye jamii kuwa magonjwa wa Ngiri maji na Matende yapo tu katika mikoa ya Pwani hali ambayo imekuwa ni tofauti baada ya tafiti zilizofanyika na kuweza kubaini kuwa mikoa yote nchini ina waathirika wa magonjwa hayo.
"Tulifanya tafiti katika halmashauri zote nchini 184 na kuona katika halmashauri 119 wapo watu ambao tayari walikuwa wameathirika au kuwa na vimelea na jitihada za kuhakikisha maambukizi hayaendelei katika halmashauri zote hizo zimeazaa matunda na sasa hivi bado tuna halmashauri tisa tu ndio ambazo bado tunaendelea kugawa dawa za kinga kwaajili ya kutokomeza maambukizi ya ugonjwa wa matende na mabusha na kwa walioathirika wako katika halmashauri zote na kule ambako maambukizi yalionekana kuwa makubwa ndiko ambako tunao watu wengi waliopata madhara" alisema Dokta Faraja.
"Mpaka sasa hivi tangu tumeanza kambi hizi za upasuaji kwa Tanzania maeneo yote tumeshafanya upasuaji zaidi ya watu elfu kumi na tunakadiria wengine elfu kumi ambao bado wana uhitaji, na ugonjwa huu ulijengeka kuwa labda uko maeneo ya pwani peke yake kitu ambacho hakikuwa sahihi ukweli ni kwamba ugonjwa huu upo kila mahali ambapo kuna mbu wanaweza kueneza ugonjwa huu"
Aidha dokta Faraja alisema kuwa lengo la wizara kupitia mpango huo wa taifa wa kudhibiti magonjwa ambayo hayapewi kipaumbele bado elimu inaendelea kutolewa kwa wananchi kupitia njia mbalimbali hii ikilenga kuongeza uelewa na kuhamasisha wagonjwa kufika katika vitu vya afya zinakopatikana huduma hizo ili kupatiwa matibabu.
Mganga mkuu wa mkoa wa Tanga Japhet Simeo ameleza kuwa tayari huduma hiyo ya upasuaji wa ngirimaji imeshafika katika wilaya z Pangani Muheza na Mkinga na wagonjwa elfu moja walishaifanyiwa upasuaji huku wakitarajia kuwafikia wengine 100 kwa siku tano ambazo kampeni hiyo inafanyika ndani ya jiji la Tanga.
"Kwa mkoa wa Tanga maeneo ambayo tayari wameshapatiwa huduma ni Muheza Pangani na Mkinga na zaidi ya watu elfu moja wameshapatiwa huduma hii na tunatarajia kutoa huduma kwa watu wasiopungua mia moja baada ya kampeni tuliyoweka kwa siku hizi tano kutakuwa na vifaa ya kuweza kuhudumia watu mia tatu katika vituo vinne ambavyo ni kwenye halmashauri za Mkinga Pangani na Muheza " alisema Simeo.
Alisema kuwa tatizo la magonjwa ya Ngirimaji pamoja na yale ambayo hayapewi kipaumbele bado ni kubwa huku wagonjwa wakikabiliwa na unyanyapaa katika jamii huku wakijiapanga kuendelea kutoa elimu zaidi kwa jamii pamoja na kuhamasisha wagonjwa kujitokeza katika vituo vya afya ili kuweza kupatiwa matibabu bure.
"Tatizo bado ni kubwa kwa jinsi ambavyo hawapewi kipaumbele na ukiangalia waliokwishapata huduma ni wale waliopata ujasiri wa kujitokeza kwenye matibabu kwahiyo inawezekana tatizo ni kubwa tofauti na tunavyoweza kuliona na tunaokutana nao, changamoto ya tatizo hili inaambatana na unyanyapaa kwa mgonjwa binafsi lakini jamii inaweza ikamnyanyapaa" aliongeza
Baadhi ya wagonjwa ambao tayari wameshafanyiwa upasuaji wa Ngiri maji waliopo katika kituo cha afya Mwakidila jijini Tanga akiwemo Mussa Mashaka waliishukuru na kuipongeza serikali kwa msaada huo walioupata bure wakieleza kuwa bado tatizo lipo katika jamii akiwahamasisha wengi kujitokeza kupata matibabu hayo.
"Ninashukuru sana serikali kwa hili kwa sababu hizi huduma ukizihitaji hospitalini gharama yake ni kubwa changamoto kubwa ni kuficha ugonjwa huu kwenye jamii unapoon watu mbele yako unakosa raha kabisa hasa nyumbani kunapokuwa na shughuli, naombeni sana jamik mwenye tatizo kama hili hii fursa tuitumieni vizuri tu" alisema Mashaka
Kwa upande wake Ally Boza aliyesumbuliwa na ugonjwa wa Ngirimaji kwa muda wa miaka minne ameishukuru serikali kwa kupata huduma ya oparesheni bure akiiomba kuzidi kutoa elimuzidi huku akibainisha kuwa ugonjwa huo wengi katika jamii wamekuwa wakiuhusisha na imani potofu.
"Nina mwaka wa nne maradhi haya ninayo kiukweli wengi walikuwa wanasema ni uchawi lakini mimi niwaambie tu kwamba sio uchawi Ngirimaji ni maradhi kama maradhi mengine na inatibika kama kawaida ugonjwa huu wengi tulikuwa tunahitaji tupate huduma lakini uwezo hatuna , tunazidi sana kuishukuru serikali huduma n nzuri sana nahamasisha na wengineo waje" alisema Boza.
Kampeni hiyo ya kudhibiti magonjwa yasisyopewa kipaumbele ikiwemo Ngiri maji na Matende bado inaendelea nchi nzima kwa wagonjwa kujitokeza kayika vituo vya afya kufanyiwa upasuaji na kupatiwa dawa bure
Post A Comment: