Vijana kutoka Kaya maskini na wanaoishi katika mazingira magumu hapa nchini wameshauriwa kuchangamkia fursa za Mafunzo ya Kukuza na Kuendeleza Ujuzi yanayotelewa na Serikali kupitia vituo mbalimbali vya Mafunzo ya Elimu ya Ufundi na Ufundi Stadi.
Ushauri huo umetolewa Kisiwani Unguja - Zanzibar na Mkurugenzi wa Utafutaji Rasilimali na Usimamizi wa Miradi kutoka Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA) Bw. Waziri Salum alipokuwa katika ziara ya siku mbili ya kutembelea wanafunzi kutoka Kaya maskini wanaosoma mafunzo ya Ujuzi kupita Mpango wa Ufadhili kwa Vijana kutoka Kaya Maskini na Wanaoishi katika Mazingira magumu.
Mkurugenzi Waziri alisema Serikali inawatambua na kuwathamini vijana hao na iko tayari kuwasidia waweze kujikwamua kiuchumi na kujihusisha katika shughuli mbalimbali za ujasiriamali na uzalishaji mali aidha kwa kujiajiri wenyewe au kuajiriwa ili wajipatie kipato.
Waziri aliweka bayana kwamba, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kushirikiana na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ilizindua rasmi Mpango wa Ufadhili kwa Vijana kutoka Kaya Maskini na wanaoishi Katika Mazingira Magumu mwezi Disemba mwaka 2022 kwa lengo la kutoa Mafunzo ya Ujuzi kwa vijana 600 kutoka kaya maskini katika visiwa vya Unguja na Pemba.
Aliongeza kwamba, amefarijika kuona vijana hao wanavyojituma na kuweka bidii kwenye masomo yao na kuwaasa wasikate tamaa ya kupambania kile wanachokiamini kwani watazifikia ndoto zao za kujikwamua kiuchumi na kujipatia kipato.
Awali Mkurugenzi Waziri alisema, wakati mafunzo hayo yanazinduliwa hawakujua kama wangepata wanafunzi wa makundi gani ila baada ya mafunzo kuanza vijana walemavu na wenye mahitaji maalum ni miongoni mwa waliopata fursa ya kusoma mafunzo hayo ya ujuzi kupitia Mpango wa Ufadhili kwa Vijana Kutoka Kaya Maskini.
“Fursa bado zipo na Serikali bado inawakumbuka, mkimalimaliza masomo jiungeni kwenye vikundi na mjisajili mfanye kazi kwa umoja ili muweze kuzifikia fursa nyingi zaidi, alisema Waziri”
Aidha Mkurugenzi Waziri alitoa ahadi ya kununua cherehani moja kwa mwanafunzi mlemavu wa miguu kutoka Chuo cha Elimu Mbadala Forodhani ambaye anatumia cherehani maalum baada kuona jinsi anavyojitahidi kusoma na kujifunza kushona licha ya ulemavu alio nao,
Mwanafunzi huyo Rukia Haji Amiri alimshukuru sana Mkurugenzi kwa ahadi hiyo na kusema yeye anatoka kaya maskini na hawezi kutembea kwa hiyo hata alivyochaguliwa kujiunga na masomo bado hakuwa na jinsi ya kufika darasani kwa hiyo ilimlazimu amuombe ndugu yake mtoto wa shangazi yake awe anampeleka darasani asubuhi na kumrudisha jioni.
Rukia alisema, alikuwa na mawazo sana baada ya masomo angefanyaje kazi kutokana na hali yake hivyo upatikanaji wa cherehani yake ni faraja na ni ukombozi kwake kwani ana uhakika wa kufanya kazi akimaliza masomo.
Jumla ya Vijana 600 walikusudiwa kunufaika na Mpango wa Ufadhili kwa Vijana Kutoka Kaya Maskini na Wanaoishi katika Mazingira Magumu Visiwani Unguja na Pemba na mafunzo hayo yanatolewa katika vituo 9 vya Mafunzo ya Amali visiwani humo.
Post A Comment: