Na Immaculate Makilika – WHMTH
Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan imeendelea kuwekeza katika Teknolojia Habari na Mawasiliano (TEHAMA) nchini kwa lengo la kutatua changamoto ya mawasiliano ikiwa ni pamoja na kuvutia uwekezaji na kurahisisha utoaji huduma kwa wananchi.
Ni dhahiri kuwa huduma za mawasiliano ni za msingi katika maisha ya wananchi kwa vile zinagusa nyanja za kijamii, kiuchumi na kisiasa. Pia, mawasiliano yanawezesha na kuhimili sekta mbalimbali ikiwemo afya, elimu, kilimo, uwekezaji na biashara, ajira, benki na utalii kwa kuziongezea ufanisi wa kiutendaji sambamba na kutoa mchango mkubwa katika uchumi wa moja kwa moja kupitia sekta hizo.
Hivi karibuni Naibu Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Mhandisi Kundo Mathew wakati akiwa katika ziara yake ya kukagua miradi ya mawasiliano, ubora na upatikanaji wa huduma za mawasiliano, usikivu wa redio TBC Taifa na uhakiki wa Anwani za Makazi katika Wilaya ya Mafia Mkoa wa Pwani anasema kuwa Mhe. Rais Dkt. Samia amefanya kazi ya kimapinduzi ndani ya Wizara yake ambayo inabeba miundombinu yote ya kimawasiliano nchini kwa kuiongezea bajeti yake ili iweze kuakisi uhalisia wa kazi adhimu inayotakiwa kufanyika katika masuala ya TEHAMA nchini.
‘‘Bajeti ya wizara hii ilikuwa shilingi bilioni nane kwa mwaka lakini Mhe. Rais alivyoingia madarakani kwa awamu yake ya kwanza alipitisha bajeti ya shilingi bilioni 230,” anasema Mhe. Naibu Waziri Kundo.
Anasisitiza: “Shilingi bilioni 230 maana yake ni miradi mingi zaidi ya ujenzi wa miundombinu ya mawasiliano, ajira za moja kwa moja, na miundombinu inapoimarika zaidi huduma za mawasiliano zinazidi kupatikana kwa urahisi na gharama zake zitaendelea kuwa nafuu.”
Sambamba na hayo, Mhe. Naibu Waziri kundo, amebainisha kuwa kati ya jitihada zinazofanywa na Serikali za uwekezaji wa miundombinu ya TEHAMA ambapo katika bajeti ya mwaka 2022/23 Serikali imetoa shilingi bilioni 145 kwa ajili ya ujenzi wa Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano.
Aidha, hadi sasa Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano umeunganishwa na nchi jirani ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo ili uweze kutoa huduma pamoja na maeneo mengine ya mpakani.
Fauka ya hayo, Juni 26, 2021, Serikali kupitia aliyekuwa Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Dorothy Gwajima ilizindua Mpango Mkakati wa Sekta ya Afya wa Awamu wa Tano katika mkutano ulioshirikisha wadau mbalimbali wa sekta hiyo ambapo alieleza kuwa Mpango Mkakati huo umejielekeza kuleta matokeo katika maeneo matano ya kimkakati.
Ambayo ni kuimarisha upatikanaji wa huduma za afya kwa kuendelea kujenga miundombinu, kuongeza watumishi, vifaa tiba, dawa na vitendanishi, kuimarisha utayari wa kujiandaa na kukabiliana na magonjwa ya mlipuko na dharura kwa kuboresha mfumo wa kutoa taarifa ya viashiria hatarishi, ushirikishwaji wa jamii, usafi wa mazingira.
Pamoja na udhibiti wa taka hatarishi, upatikanaji wa fedha, mabadiliko chanya ya tabia na ushirikishwaji wa sekta nyingine.
‘‘Eneo la tatu ambalo Serikali imejielekeza ni kuendelea na jitihada za kuboresha kitita cha huduma za Afya katika ngazi ya msingi na huduma za rufaa, huduma za utengamao, huduma za shufaa, huduma za tiba asili na tiba mbadala. Aidha, katika eneo hili Sekta ya Afya itaendelea kuimarisha huduma za matibabu ya kibingwa na kuzipeleka huduma hizi kwenye Hospitali za Rufaa za Mikoa’’. Anasema Waziri Gwajima.
Maeneo mengine ya kimkakati yanatajwa kuwa ni kuimarisha uhusiano wenye matokeo chanya wa kiutendaji wa mifumo ya afya katika kuongeza wigo wa utoaji wa huduma, uboreshaji wa huduma, huduma za uchunguzi, huduma za damu salama, huduma za uchunguzi wa bidhaa ili kumlinda mlaji.
Ikiwa ni pamoja na kuendelea kuwekeza katika kuimarisha mifumo ya afya hususani katika rasilimali watu katika sekta ya afya, dawa na bidhaa za afya, miundombinu, TEHAMA, utafiti, katika sekta ya afya uimarishaji wa ushirikiano na sekta binafsi na rasilimali fedha.
Kuhusu utekelezaji wa baadhi ya mikakati hiyo ya TEHAMA katika Sekta ya Afya, Mratibu wa Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) Kanda ya Pwani, Mhandisi Baraka Eliezer anasema kuwa UCSAF inatekeleza mradi muhimu wa Tiba Mtandao ambao unaunganisha hospitali katika mtandao mmoja na kuhakikisha hospitali zenye huduma bora zaidi zinasaidia zile ambazo hazina wataalamu wa kutibu magonjwa bobezi na vifaa vya kisasa kwa njia ya mtandao bila kumlazimu daktari aliyekuwepo kwenye hospitali za taifa za rufaa kwenda kwenye hospitali za mikoa au wilaya.
Ambapo hivi karibuni Serikali imetumia takribani shilingi bilioni mbili katika ujenzi wa miundombinu ya kuweza kuziunganisha hospitali za mikoa na za rufaa ikiwa ni azma yake ya kuboresha sekta ya afya nchini kwa kutumia TEHAMA.
‘‘Kupitia TEHAMA daktari bingwa mbobezi wa kutibu masuala ya neva kutoka Taasisi ya Mifupa Muhimbili (MOI) anaweza kutoa huduma katika hospitali zilizopo mikoani bila mgonjwa kusafirishwa kwenda MOI, Dar es salaam. Mradi huu tulianza kuutekeleza miaka miwili iliyopita na tuliona hili ni eneo muhimu sana na linaenda sambamba na lengo letu la kuhakikisha jamii inanufaika na TEHAMA’’ anasema Mhandisi Eliezer.
Aidha, Mhandisi huyo ameishukuru Serikali ya Awamu ya Sita kwa kuhakikisha kwamba UCSAF inaendelea kupata fedha zinazowezesha kuwa na miundombinu ya Tiba Mtandao katika hospitali mbalimbali nchini.
Katika upande wa Zanzibar, Mhandisi Eliezer anasema “Serikali kupitia UCSAF inatekeleza mradi mkubwa wa Tiba Mtandao ili kutatua changamoto za kutoa huduma za kibingwa kwa kuziunganisha Hospitali za Abdallah Mzee iliyopo Pemba na Mnazi Mmoja iliyopo Unguja pamoja na Hospitali za MOI na Jakaya Kikwete. Mradi huu unategemewa kukamilika kabla ya mwezi Juni 2023, tukiamini kuwa ni mradi utakaoleta mapinduzi makubwa katika Sekta ya Afya kwa upande wa Zanzibar”.
Aidha, Mhandisi huyo anafafanuwa kuwa mfumo wa afya uliopo unailazimu Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kutumia gharama kubwa kwa mgonjwa anapotoka Zanzibar kwenda kupata huduma za rufaa Tanzania Bara na hivyo UCSAF itahakikisha huduma zote za rufaa zinapatikana pia katika Hospitali hizo za Abdallah Mzee na Mnazi Mmoja zilizopo Zanzibar.
Post A Comment: