Na Mashaka Mhando - Lushoto
TAASISI ya Maendeleo wilayani Lushoto ya Usambara Development Initiative (UDI), imejipanga kutoa elimu kwa wazazi njia bora ya kuwasimamia watoto wa kike ili wapate elimu badala ya kwenda kutafuta kazi za ndani.
Akizungumza mara baada ya kuchaguliwa mwishoni mwa wiki, Mwenyekiti wa UDI, Anna Gogola, alisema lengo kubwa ya kutoa elimu hiyo ni kukomesha dhana kwamba wilaya ya Lushoto ndiyo inayotoa mabinti wa kazi za ndani.
Alisema pamoja na UDI kugusa nyanja mbalimbali za maendeleo lakini pia watahakikisha watoto wa kike wanapata masomo yao kisha waweze kutimiza ndoto zao katika maisha.
"UDI ipo kwa ajili ya maendeleo ya Wana-Lushoto, tutahakikisha tunagusa nyanja zote, kuna dhana imejengeka Lushoto kunapatikana wadada wa kazi za ndani, tunataka kuondoa hiyo dhana," alisema Gogola.
Alisema watatumia mbinu mbalimbali ikiwemo kukaa na wazazi ili wawaeleweshe kamba upo umuhimu wa mtoto kusoma kwa kusimamiwa na wazazi badala ya kuwaacha wakafanye kazi za ndani.
Alisema serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan, imeweza kuweka miundombinu bora ambayo watoto wanasoma bure hadi Sekondari.
Alisema Kuna tabia ya wazazi kuwafanya mtaji mabinti wa kike kwa kuwafungisha ndoa mara tu baada ya kumaliza darasa la saba na wakati mwingine kumwambia mtoto afanye mtihani vibaya ili asiweze kwenda Sekondari.
"Tunataka mtoto wa Lushoto au mzazi ajue kwamba kila mtoto anapaswa kupata elimu na anapaswa kusimamiwa ili apate elimu na kutimiza ndoto zake, na siyo kufanyishwa kazi au kuwa mdada wa kazi," alisema Mwenyekiti huyo.
Mkuu wa wilaya ya Lushoto Kalist Lazaro akizungumzia kuhusu hilo, alisema kwamba serikali ikishirikiana na taasisi zisizo za kiserikali wanasaidiana katika nyanja mbalimbali ikiwemo suala la kuwataka watoto wasome na wawepo madarasani.
Alisema ameweka mkakati ambao pengine hautawapendeza wazazi wengi lakini anafanya hivyo ili kukomesha tabia ya wazazi wanaowafanya watoto wa kike mtaji.
Alisema ipo tabia ya wazazi kufika kituo cha polisi kulalamika kwamba hawawaoni mabinti wao wiki moja baada ya shule kufungulia tabia ambayo anataka kuipiga vita.
"Kuanzia Januari wazazi watakuja kusema mtoto amepotea au haonekani, lakini tangu Novemba, Desemba mtoto alikuwa hayupo hajatoa taarifa kukwepa kushitakiwa, mtoto hawezi kupotea bila mzazi kujua," alisema Mkuu huyo wa wilaya.
Alisema ikifika kipindi hicho ametoa agizo kwamba kama mtoto aliyefaulu mwenda Sekondari kisha haonekani darasani, mzazi atakaa yeye darasani hadi mwanafunzi huyo atakapopatikana.
Awali akitoa salamu aliyekuwa Mwenyekiti wa UDI Ally Daffa alisema anashukuru taasisi hiyo imepata usajili mikononi mwake na akawataka wanachama kumpa ushirikiano Mwenyekiti mpya ili umoja huo uweze kusonga mbele kwa Maendeleo ya Lushoto.
Katika hatua nyingine, Ofisa Habari na mahusiano wa UDI Esther Kiondo, aliwataka wakazi wa Lushoto popote walipo nchini kujiunga na umoja huo ili kushughulikia kwa pamoja changamoto mbalimbali zinazoikabili wilaya hiyo.
Post A Comment: