Na Mwandishi Wetu
Mkurugenzi wa Huduma za Ajira, Ofisi ya Waziri Mkuu , Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Joseph Nganga, amezishauri nchi za ukanda wa Mashariki na Pembe ya Afrika kuongeza ushirikiano ili rai wa nchi hizo wanufaike na fursa za ajira zinazojitokeza.
Akizungumza kwa niaba ya Serikali ya Tanzania kwenye mkutano wa Kanda hiyo unaofanyika Zanzibar Januari 24 hadi 25, 2023, Nganga amesema ushirikiano wa nchi hizo utaongeza ufanisi katika kuwezesha ajira za staha kwa raia wake.
“Nashauri nchi hizi kuweka utaratibu wa kujadili na kuingia makubaliano na nchi zenye fursa za ajira kama ukanda, kutekeleza programu za kuwajengea ujuzi stahiki raia wanaoenda kufanya kazi nje ya ukanda.”
“Kuweka mifumo ya kielektroniki kuratibu michakato ya uhamaji nguvukazi, pamoja na kukusanya, kuchambua takwimu na kutoa taarifa za uhamaji nguvukazi,”amesema.
Aidha, amsema uhamaji nguvukazi ni jambo linaloendelea kukua kutokana na kupanuka kwa mashirikiano ya kikanda pamoja na maendeleo ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano.
Aidha, amesema uhamaji wa nguvukazi una mchango mkubwa katika maendeleo ya nchi husika kwa kuongeza fursa za ajira na hivyo kukuza uchumi wa nchi husika.
Mkutano huo umeshirikisha nchi za Kenya, Tanzania, Somalia, Ethiopia, Uganda, Djibouti, Sudan Kusini na Sudan na unalenga kubadilishana uzoefu na kuweka mikakati ya pamoja kuhusu masuala ya uhamaji nguvukazi.
Post A Comment: