Uongozi wa Taasisi ya Moyo  Jakaya Kikwete (JKCI-Dar Group) umetakiwa kujikita kwenye utoaji wa huduma za matibabu ya moyo kwa watoto walio chini ya umri wa miaka 15.


Agizo hilo limetolewa na Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu mara baada ya kutembelea Hospitali hiyo ambayo sasa ipo chini ya usimamizi wa Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) iliyopo Jijini Dar Es Salaam.

“Hapa nataka tujikite kwenye matibabu ya moyo kwa watoto walio chini ya miaka 15 tusitoke kwenye huduma ya moyo kama ilivyokuwa malengo ya Taasisi ya Moyo JKCI” amesema Waziri Ummy Mwalimu akitoa agizo hilo kwa Uongozi wa Taasisi ya JKCI.

Amesema kuwa rufaa zote za watoto wenye matatizo ya moyo zinatakiwa kwenda JCKI Dar Group badala ya Taasisi ya Moyo JKCI iliyopo Muhimbili ili kupunguza msongamano wa wagonjwa katika eneo moja wakisubiri kupata huduma.

Waziri Ummy amesema kuwa Hospitali ya Dar Group ipo katika mazingira rafiki kufikika kwa wakazi wa Wilaya za Temeke, Ilala na Kinondoni lakini hata kwa wageni wanaofika katika Mkoa wa Dar Es Salaam kwa usafiri wa treni au anga hivyo kuagiza Hospitali hiyo kuboresha zaidi huduma zinazotolewa ili kuvutia watu kufika hapo kupata huduma.

Amesema kuwa agizo hilo haliathiri utolewaji wa huduma nyinginezo ambazo zinaendelea kutolewa ila mwelekeo wa Hospitali hiyo utajikita kwenye umahiri wa utoaji wa matibabu ya kibingwa ya moyo.

Aidha Waziri Ummy ameagiza pia Taasisi hiyo kusogeza zaidi huduma za matibabu ya kibingwa ya Moyo katika Kanda ya Ziwa katika Hospitali ya Rufaa ya Kanda Chato pamoja na Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Kusini Mbeya huku akiagiza kituo cha Morogoro kufungwa ili kuongeza nguvu katika Hospitali ya Dar Group pamoja na Hospitali ya Rufaa ya Kanda Chato.

Awali akizungumza Mganga Mkuu wa Serikali Prof. Tumani Nagu ameipongeza Taasisi ya JKCI kwa kuipokea Hospitali ya Dar Group kwa vitendo na kuanza maboresho ya huduma kwa haraka katika kipindi cha miezi miwili.

 Prof. Nagu amesema kuwa ni dhamira ya Serikali kupambana na magonjwa yasiyoambukiza hivyo Taasisi hiyo ina mchango mkubwa katika kutibu na kutoa elimu ya kujikinga dhidi ya magonjwa yasiyoambukiza hivyo usimamizi wa Hospitali ya Dar Group chini ya JKCI kutasogeza karibu huduma za matibabu ya kibingwa ya moyo kwa wananchini.

Prof. Nagu amesema pamoja na kupanua wigo wa huduma, Serikali itaendelea kuhimiza ubora wa huduma zinazotolewa katika vituo vya kutolea huduma za afya nchini.

“Tuangalie ubora wa huduma kwa kuangalia mahitaji ya mteja, mteja anataka huduma salama, bora na inayopatikana kila wakati kwa haraka na haya ndio mambo ambayo tunasisitiza kila siku” amefafanua Prof. Nagu.

Hapo awali Hospitali ya Dar Group ilijengwa kwa ajili ya kutoa Huduma za Afya kwa wafanyakazi wa Viwandani na kusimamiwa na Msajili wa Hazina. 

Mnamo mwezi Novemba 2022 Serikali kupitia Wizara ya Fedha, Msajili wa Hazina walifanya maamuzi ya kuichukua Hospitali hiyo na kuipatia Wizara ya Afya kwa ajili ya usimamizi na kutatua changamoto za kiutendaji zilizokuwepo hapo awali.








Share To:

Post A Comment: