Serikali kupitia Wizara ya Katiba na Sheria imeihakikishia Mahakama ya Afrika inayoshughulika na haki za binadamu kuwa inathamini mchango mkubwa unaotolewa na na mahakama hiyo katika kulinda na kutetea haki za binadamu na kwamba ipo tayari kushirikiana mahakama hiyo katika kushughulikia masuala yote yahusuyo haki za binadamu.
Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Dkt. Damas Daniel Ndumbaro (Mb) jana tarehe 11, Januari 2022 Jijini Dar es Salaam alipokutana na kufanya mazungumzo na Rais wa Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu Mhe. Jaji Iman Daudi Aboud huku akibainisha mipango ya Serikali katika kuchangia upatikanaji wa haki za binadamu.
Aidha katika mazungumzo yao, Waziri Ndumbaro ameeleza kuwa Serikali inachukulia kwa uzito mkubwa uwepo wa Mahakama hiyo nchini ikizingatiwa kuwa Serikali inayoongozwa na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan imeyapa umuhimu na uzito mkubwa masuala yote yahusuyo haki za Binadamu.
Jaji Aboud amefika kufanya mazungumzo kuhusu masuala mbalimbali yahusuyo Haki za Binadamu nchini na namna bora ya kuendeleza ushirikiano kati ya Serikali na Mahakama hiyo ambapo kwa upande wa serikali, Mhe. Ndumbaro alisema wizara yake kwa kushirikiana na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki inaendelea kufanya mchakato wa ujenzi wa jengo la kudumu la Mahakama hiyo na kwamba amepanga kuitembelea mahakama hiyo hivi karibuni.
Kikao hicho pia kilihudhuriwa na Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Haki za Binadamu Bw. Richard Kilanga kutoka Wizara ya Katiba na Sheria, Bw. Hangi Chang’a Mkurugenzi Msaidizi sehemu ya Katiba, Haki za Binadamu na Mashauri ya Uchaguzi na Bi. Vivian Method Wakili wa Serikali Mwandamizi wote kutoka Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali.
Mtanzania Jaji Imani Daud Aboud ambaye pia ni Jaji wa Mahakama Kuu nchini Tanzania aliteuliwa Mei 2021 kuwa Rais wa Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu Watu yenye Makao yake Makuu jijini Arusha. Jaji Imani amekuwa mwanamke wa pili kushika wadhifa huo mkubwa katika mahakama hiyo.
Post A Comment: