Na Magesa Magesa,Arusha
SERIKALI Mkoani Arusha imejipanga kikamilifu kuhakikisha kuwa
inakabiliana na vitendo vyote vile vinavyoenda kinyume na maadili
katika shule zote za msingi na sekondari zilizopo Mkoani hapa.
Afisa Elimu wa Mkoa wa Arusha,Abel Mtopwa aliyasema hayo juzi
alipokuwa akizungumza na wanahabari ofisini kwake na kuongeza kuwa
jukumu hili sio la kuiachia serikali peke yake kwani ni la jamii kwa
ujumla.
“Ni jukumu la wazazi/walezi na waalimu kuhakikisha kuwa wanasimamia
kikamilifu nidhamu kwa wanafunzi na kuhakikisha kuwa wanakemea matendo
yote yale yanayoenda kinyume na maadili ya mtanzania kwa
wanafunzi”alisema
Mtopwa aliyasema hayo kufuatia hivi karibuni kuripotiwa taarifa ya
baadhi ya wanafunzi kufundishwa vitendo vya kulawitiana ambavyo ni
kinyume na maadili katika baadhi ya shule zilizopo katika mkoa wa
jirani wa Kilimanjaro.
Alisema kuwa Mkoa wa Arusha umechukua taadhari zote kukabiliana na
matukio hayo na kwamba mpaka sasa hakuna shule hata moja iliyoripotiwa
kujihusisha na matukio hayo na kwamba wameishatoa maagizo kwa waalimu
wakuu na maafisa elimu wa kata juu ya matukio hayo.
Afisa elimu huyo alitoa wito kwa wazazi kuhakikisha kuwa kila mtoto
amnayehitajika kwenda shule wahakikishe kuwa anaripoti kwani kwa sasa
hakuna kisingizio chochote ukizingatia kuwa serikali imeweka mazingira
mazuri ya kujisomea pamoja na kutoa elimu bure kuanzia darasa la
kwanza hadi kidato cha sita.
“Nitoe wito kwa wazazi kuhakikisha kuwa wanachangia kwa hiari chakula
cha mchana kwa nanafunzi kwa mujibu wa waraka wa elimu namba 6 wa
mwaka 2016 kwani jukumu la kumpa mtoto chakula,sare na vifaa vyote
vya kujifunzia ni la mzazi”alisema.
Afisa elimu huyo wa Mkoa alisema kuwa mkoa wa Arusha ulitarajia
wanafunzi elfu 4288 kujiunga na kidato cha kwanza kwa mwaka huu wa
2023 na kwamba mpaka sasa wanafunzi elfu 3274 sawa na 75%
wamekwishajiunga na kuwataka wale wote ambao hawajaripoti kuripoti
shuleni mara moja.
Post A Comment: