Kamishna wa Sera wa Wizara ya Fedha na Mipango, Bw. Elijah Mwandumbya, akizungumza jijini Dodoma na wanahabari kuhusu Kongamano la kwanza la Kodi Kitaifa lenye lengo la kuongeza ushiriki wa wadau kwenye maboresho ya sera za kodi, linalotarajiwa kufanyika Januari 11, 2023 jijini Dar es salaam katika ukumbi wa JNICC.
Na. Farida Ramadhani na Haika Mamuya, WFM – Dodoma
Serikali kupitia Wizara ya Fedha na Mipango imeanzisha Kongamano la Kodi Kitaifa litakalowashirikisha wadau mbalimbali ikiwemo Sekta Binafsi ili kajadili namna ya kuboresha Sera za Kodi, kuchochea ukuaji wa uchumi, biashara na uwekezaji nchini.
Hayo yameelezwa na Kamishna wa Sera kutoka wizara hiyo, Bw. Elijah Mwandumbya, katika mkutano na wanahabari ulifanyika jijini Dodoma.
Bw. Mwandumbya alisema Kongamano hilo litarahisisha zoezi la ukusanyaji wa maoni ya wadau kwa ajili ya maboresho mbalimbali ya Sera za Kodi na kuongeza ushirikishwaji wa makundi hayo katika utunzi wa sheria.
“Serikali Kupitia Wizara ya Fedha na Mipango, ina jukumu la kuratibu upatikanaji wa maoni ya wadau, kuchakata maoni hayo na hatimaye kuyawasilisha kwenye Kamati ya Ushauri wa Kodi, mapendekezo mbalimbali ya sera za kodi yanayotarajiwa kufanyika kwa mujibu wa Kifungu cha 10(1) cha Kanuni za Bajeti za mwaka 2015”, alibainisha Bw. Mwandumbya.
Alisema katika kongamano hilo litakalokutanisha wataalam wa uchumi, fedha na kodi nchini, mada mbalimbali zitawasilishwa na kujadiliwa ikiwa ni pamoja na hali ya uchumi duniani, fursa na athari zake kwenye sera za uchumi, uwekezaji na biashara nchini.
Bw. Mwandumbya aliongeza kuwa mada nyingine zitakazowasilishwa na kujadiliwa ni mfumo wa kodi, ada na tozo mbalimbali pamoja na hali ya ulipaji kodi kwa hiari na changamoto zake katika mazingira ya uchumi, biashara na uwekezaji nchini.
Alibanisha kuwa Kongamano hilo la kipekee pia litajadili mchango wa sekta ya fedha katika kukuza uchumi, biashara na uwekezaji wakati huu wa changamoto za uchumi duniani.
Aidha alitoa rai kwa waalikwa wote wa Kongamano hilo litakalofunguliwa na Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba Januari 11, 2023, katika ukumbi wa JNICC Jijini Dar es Salaam, kushiriki kikamilifu katika kutoa michango na maoni yao ili kufankisha malengo yaliyokusudiwa.
Baadhi ya maafisa wa Wizara ya Fedha na Mipango waliohudhuria mkutano wa waandishi wa Habari na Kamishna wa Sera, Bw. Elijah Mwandumbya, kuhusu Kongamano la kwanza la Kodi Kitaifa lenye lengo la kuongeza ushiriki wa wadau kwenye maboresho ya sera za kodi, linalotarajiwa kufanyika Januari 11, 2023 jijini Dar es salaam katika ukumbi wa JNICC .
Kamishna wa Sera Wizara ya Fedha na Mipango, Bw. Elijah Mwandumbya (kulia) akiwa na Kamishna Msaidizi wa Sera, Bw. Willium Muhoja, katika mkutano wa waandishi wa Habari na Kamishna huyo, kuhusu Kongamano la kwanza la Kodi Kitaifa lenye lengo la kuongeza ushiriki wa wadau kwenye maboresho ya sera za kodi, linalotarajiwa kufanyika Januari 11, 2023 jijini Dar es salaam katika ukumbi wa JNICC.
Baadhi ya Wanahabari waliohudhuria katika mkutano wa Waandishi wa Habari na Kamishna wa Sera wa Wizara ya Fedha na Mipango, Bw. Elijah Mwandumbya, kuhusu Kongamano la kwanza la Kodi Kitaifa lenye lengo la kuongeza ushiriki wa wadau kwenye maboresho ya sera za kodi, linalotarajiwa kufanyika Januari 11, 2023 jijini Dar es salaam katika ukumbi wa JNICC.(Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, WFM, Dodoma)
Post A Comment: