Moja kati ya malengo ya Wizara ya Kilimo kufikia mwaka 2030 yakiongozwa na Rais wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Awamu ya Sita, Dkt. Samia Suluhu Hassan ni kuendelea kutoa ruzuku ya mbolea mpaka pale itakaposhuka bei kwenye soko la dunia ili kuwapunguzia gharama za uzalishaji wakulima nchini.
Waziri wa kilimo, Hussein Bashe amesema, Serikali ya Awamu ya kwanza ya Mwl. Julius Kambarage Nyerere ni serikali pekee iliyokuwa na na maono ya muda mrefu ya kuwekeza kwenye Sekta ya Kilimo ikifuatiwa na Serikali ya Rais Dkt. Samia aliyeonesha utashi wa kisiasa wa kuwekeza kwenye Sekta ya Kilimo.
Waziri Bashe amezungumza hayo leo tarehe 10 Januari, 2022 wakati wa kikao kilichohusisha wahariri na waandishi wa vyombo mbalimbali vya habari nchini, watumishi wa wizara ya kilimo, wakuu na watumishi wa taasisi zilizopo chini ya wizara na wadau mbalimbali wa Sekta ya Kilimo ndani na nje ya nchi kilichojadili utekelezaji wa mipango ya wizara kwa bajeti ya mwaka 2022/2023 .
Ameeleza kuwa, kufuatia mfumuko wa bei ya mbolea kwenye soko la dunia msimu wa kilimo wa 2021/2022, Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan aliridhia na kuzindua mpango wa utoaji wa mbolea za ruzuku tarehe 8 Agosti, 2022 ulioanza kutekelezwa tarehe 15 Agosti, 2022.
Akizungumzia kuhusu mfumo wa kidigitali wa utoaji wa mbolea za ruzuku, waziri Bashe amesema mfumo una changamoto na kueleza changamoto mojawapo kuwa ni wakulima kutokuukubali utaratibu unaofuatwa kwenye manunuzi ya mbolea hizo kutokana na kutumia muda mrefu.
Ameeleza changamoto ya pili kuwa ni uchache wa vituo vya kuuzia mbolea na kueleza kuwa changamoto hiyo inafanyiwa kazi kwa ushirikiano baina ya ofisi za wakuu wa mikoa na wilaya kwa kubaini vituo vipya vitakavyosajiliwa na Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA) ili wakala wa mbolea waweze kufikisha mbolea katika vituo hivyo na kutatua changamoto ya wakulima kufuata mbolea maeneo ya mijini.
Amefafanua kuwa mifumo yote iliyotumika kutoa ruzuku kwa miaka iliyopita ilikuwa haijui ni nani anayenufaika na mbolea ya ruzuku lakini kupitia mfumo huu wa kidijitali unaomtaka mkulima, wakala, kituo cha mauzo, mwingizaji na mzalishaji wa mbolea kusajiliwa unatambua mnyororo mzima wa biashara ya mbolea na hivyo kuwa na uhakika wa mnufaika wa mwisho wa ruzuku iliyotolewa na serikali.
Akizungumzia walichojifunza kupitia utekelezaji wa utoaji wa mbolea za ruzuku kwa kutumia mfumo wa kidigitali, Mkurugenzi Mtendaji wa TFRA amesema mfumo ni mzuri ijapokuwa unaendelea kuboreshwa kadri changamoto na mapendekezo yanavyotolewa na wadau.
Akieleza namna bora ya kutatua changamoto ya foleni kwenye vituo vya mauzo, Dkt. Ngailo amesema mosi ni kuvihusisha vyama vya ushirika kwenye usambazaji wa mbolea za ruzuku kwa kukusanya mahitaji ya wanachama na viongozi kukusanya pesa za wanachama kulingana na mahitaji na kununua mbolea kwa pamoja kuliko mkulima mmojammoja kufuata mbolea kwenye kituo cha mauzo.
Ameeleza utatuzi wa pili kuwa ni kuwasihi wakala na waingizaji wa mbolea kuongeza idadi ya watoa huduma ili kuhudumia wakulima kwa haraka kuliko kuwa na watoa huduma wachache hususan katika msimu huu wa kilimo.
Aidha, Dkt. Ngailo amesema, maboresho ya mfumo wa ruzuku yanaendelea kadri changamoto zinavyojitokeza na kueleza huko mbele wakulima watakuwa wakitumia alama za vidole wakati wa kununua mbolea ili kupunguza udanganyifu kwenye biashara ya mbolea.
Amebainisha kuwa, kufuatia uwepo wa mbolea ya ruzuku kwa msimu huu wa kilimo kumekuwa na ongezeko kubwa la matumizi ya mbolea ikiwa ni ishara ya kuongezeka kwa maeneo ya kilimo na matumizi ya mbolea ukilinganisha na msimu uliopita wa kilimo.
Post A Comment: