Na. OMM Rukwa

 

Serikali imewataka wananchi kutouza vifaa vya msaada walivyopatiwa na kufuatia maafa ya upepo mkali uliosababisha  nyumba 45 kuezuliwa na baadhi kubomoka katika kijiji cha Tamasenga kata ya Pito wilaya ya Sumbawanga mwaka jana.

 

Kauli hiyo ya serikali imetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Queen Sendiga leo ( Januari 03,2023) wakati akikabidhi msaada wa vifaa vya kibinadamu vilivyotolewa na Ofisi ya Waziri ya Waziri Mkuu Idara ya Menejimenti ya Maafa  kufuatia kuathirika na upepo mkali  hapo Desemba 16, 2022.

 

Akizungumza  kwenye hafla ugawaji wa vifaa hivyo, Sendiga alionya kuwa wananchi watakaobainika kuuza vifaa hivyo wajue wanaikosea serikali hivyo itachukua hatua kali za kisheria kwa kuwa vifaa hivyo lengo lake na kusaidia kaya zilizoathirika.

 

Sendiga alitaja vifaa vitakavyokabidhiwa kwa wahanga kuwa ni mahindi tani 9.2, ndoo 223, mikeka 200, magodoro 200, blanketi za wakubwa 200, sahani 256, vikombe 256 na sufuria 220.


“Msaada huu unatakiwa kwenda kwa walengwa, leo nitakabidhi vifaa kwa Mkuu wa Wilaya ili avikabidhi kwenu. Sitotaka kusikia malalamiko  kuwa walengwa wamekosa msaada” alisema Sendiga.

 

Kwa upande wake Mratibu wa Maafa toka Ofisi ya Waziri Mkuu Doris Pantaleo alisema mwongozo wa utoaji misaada ya kibinadamu ambao kila mmoja anapaswa kuuzingatia wakati wa utoaji misaada hiyo.

 

Naye mkazi wa kijiji cha Tamasenga Frolence Maongezi alisema ni wakati muafaka kwa wananchi wa maeneo hayo kuanza kupanda miti kwenye makazi yao ili kujikinga na madhara ya upepo mkali ambao mara kwa mara umekuwa ulisababisha maafa.

 

Jumla ya  kaya 45 zenye wakazi 256 walioathirika kwenye maafa hayo ya kijiji cha Tamasenga wilaya ya Sumbawanga wamekabidhiwa msaada huo wa serikali ambapo wito umetolewa kwa wananchi kuendelea kuwasaidia.

Share To:

Post A Comment: