BARAZA la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) limesaini mkataba wa kuangalia ubora wa maji, viwango vinavyoingia katika Ziwa Victoria na visababishi vya uchafu wa mazingira lengo likiwa ni kuendelea kupunguza uchafu ili maji yawe safi.
Mkataba huo umesainiwa leo Dar es Salaam baina ya NEMC na Kituo cha Sayansi na Mazingira (CSE) cha nchini India.
Akizungumza, Mkurugenzi Mkuu wa NEMC, Dk Samuel Gwamaka amesema kusainiwa kwa mkataba huo ni marejeo baada ya mkataba mwingine uliosainiwa mwaka 2017 wenye uhusiano ya kushirikiana kiutafiti kubadilishana utaalam pamoja na kutengeneza kanuni miongozo na viwango vya kisheria kwa ajili ya kuboresha maandiko ya tathmini ya athari za mazingira na tathmini za ukaguzi wa miradi za maendeleo
Amesema kupitia mkataba huo, yapo maeneo mawili waliyogusia ikiwa kuendelea kufanyia utafiti ziwa Viktoria liliko jijini Mwanza ambalo linagusa nchi tatu za Afrika Mashariki lakini pia unaungana na mto Nile ambao maji yake yanazikutanisha nchi za Sudan na Misri.
“Ubora wa maji wowote unaingia pale ni moja ya mambo ya msingi yanayofanyiwa utafiti, kwa Mwanza kuna mito kadhaa inaingia kwenye Ziwa ambayo kwa sababu ya shughuli za binadam inachafua mazingira na una athari kiafya na kiikolojia, amesema Dk Gwamaka.
Dk Gwamaka amesema pia wanashirikiana na kituo hicho kutengeneza kanuni ama miongozo,ili kwamba miradi inayotekelezwa isitofautiana ubora kw akuwa maandiko yanayotolewa na wataalam yamekuwa na changamoto ya kutowiana na kuwa bora .
Amesema ni vizuri kila aina ya sekta kwa mfano ya viwanda na hata kwenye migodi kutengeneza hadidu za rejea kwa watalam waelekezi waweze kufanya maandiko ya tathmini ya athari za mazingira wakijua kabisa taarifa gani zinatakiwa na lazima ziwepo ili kufikia viwango jambo litakalosaidia wale watekelezaji wa mpango wa utunzaji wa mazingira kujua kuwajibika kutunza mazingira
Dk Gwamaka amesema uchafuzi wa mazingira kwa Ziwa Viktoria pia unatoka na shughuli za binadamu nyingi, haswa ikiwa sehemu kubwa ya nyumba zilizojengwa mkoani humo zimejengwa kwenye milima, hivyo wakati mvua uchafu hutiririka kwenda ziwani lakini pia kuna viwanda vinavyotiririsha uchafu kwenda Ziwani.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo hicho, Anumita Roychowdhury amepongeza ushirikiano kati yao na NEMC wenye dhumuni kubwa la namna ya kujenga uwezo kuhusu athari za mazingira katika Ziwa Viktoria lilipo jijini Mwanza.
Amesema wamezindua ripoti yenye miongozo kuhusu ziwa hilo ambalo linategemewa na maisha ya wananchi wengi jijini humo na ni eneo muhimu kwa ikilojia.
Post A Comment: