MBUNGE wa Viti Maalum Mariam Ditopile ametoa mifuko ya saruji 100 kwa ajili ya ujenzi wa bweni la wanafunzi katika shule maalum Kongwa kitengo cha viziwi ili kuondoa changamoto ya wanafunzi kutembea umbali mrefu.

Msaada huo umefuatia baada ya kusomwa kwa taarifa ya shule inayoonyesha  uwepo wa wanafunzi wanaoshindwa kuhudhuria masomo kutokana na umbali mrefu na wakati mwingine kupata tishio la fisi wakiwa njiani.

Akizungumza Januari 26,2023,kwenye ziara yake shuleni hapo akiwa katika maadhimisho ya kuelekea miaka 46 ya  kuzaliwa Chama Cha Mapinduzi (CCM),Mariam amesema kupitia changamoto alizozisikia ameguswa kuanzisha ujenzi wa bweni ili kuwasaidia watoto hao.

"Changamoto zenu za uhaba wa walimu,bweni nimezisikia,wakati nafanya mpango wa kufuatilia serikalini utatuzi wa hizi changamoto ni vyema na sisi tuanze,kwa kuanzia natoa mifuko ya saruji 100,"amesema.

Amewataka umoja wa vijana UVCCM mkoa wa Dodoma kukaa na kuweka mikakati ya kushiriki ujenzi huo iwe kwa michango kutoka kwa viongozi wote wa umoja huo mkoa na nguvu kazi pia.

"Uongozi mzuri ni ule unaoacha alama,hebu viongozi shirikianeni mchangishane hata 2,000 kila mmoja,tuna nguvu kazi ya kutosha kupitia vijana,njooni hapa siku moja tuanze kazi ya kuchimba msingi,tuanze ujenzi,ili hata serikali ikija kusaidia ikute tumeshaanza,"amesema.

Kwa upande mwingine Mbunge Ditopile amempongeza Rais Dkt Samia Suluhu Hassan  kwa kuruhusu mikutano ya hadhara kama namna ya kuenzi maono ya Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere na dhana ya kukiimarisha chama.

" Mimi nimefurahi mikutano hii kuruhusiwa ili wajulikane wenye pumba na mchele ni akina nani,jukumu letu ni kusimama na kusemea serikali na chama chetu,kwanza sasa hivi Rais amefanya mengi sana hata tukisimama kwenye majukwaa tuna mambo mengi ya kueleza,tuna mambo mengi ya kujivunia,"alisema.



Share To:

Post A Comment: