Mwandishi Wetu.

KILIO cha mbolea ya ruzuku chashika kasi baada ya Madiwani,  Viongozi wa Chama cha Mapinduzi Kata na Viongozi wa Matawi ya CCM  zaidi ya 250 wa Mufindi Kusini wameiangukia serikali na  kuiomba kuwapelekea mbolea hiyo ambayo imeadimika kabisa Vijijini.

Viongozi hao wameyasema hayo kwa Nyakati tofauti ikiwemo  jana Januari 2, 2023 katika kikao  cha tathmini ya utendaji katika mwaka 2022 na kuweka mkakati  wa pamoja wa kujipanga kwa maandalizi ya uchaguzi wa  serikali za mitaa 2024.

Kikao hicho kilihitishwa  na Mbunge wa Mufindi Kusini,  ambaye pia ni Mwenyekiti wa Bunge la Tanzania, David Kihenzile.

Wakiuzungumza kwenye Mkutano huo maalumu wa ndani, Viongozi hao,  kwa Umoja wao wametumia nafasi hiyo kuishukuru Serikali ya CCM inayoongozwa na Rais Dk Samia Suluhu Hassan kwa kuweka ruzuku kwenye Mbolea ambapo Mwaka huu inauzwa Shilingi  70,000 kwa Mfuko baadala ya bei ya Shilingi 130,000 iliyokuwepo Mwaka 2021

Akizungumza wakati akifungua Kikao hicho, kilichofanyika kwenye Ukumbi wa Masangula,Igowole Mwenyekiti wa CCM Wilaya Mufindi George Kavenuke alisema wananchi uhaba wa Mbolea ya ruzuku imekua changamoto kubwa inayopigiwa kelele na wananchi wa Mufindi na kuiangukia serikali isikie kilio hicho na kupeleka mbolea huko akimwagia sifa Mbunge wa Jimbo hilo David Kihenzile kwa utendaji mzuri 

"Mufindi Kusini mmepata kiongozi, mshikilieni, mbadala wa Mungai (Joseph) amepatikana, anafanya makubwa katika sekta ya barabarani, Mungai enzi zake alituita wote kama hivi na  chinja ng'ombe, tulikula na kufurahi, Kihenzile  nae hivyo hivyo huu ndio uongozi, kukaa na watu kula pamoja." Alisema 

Naye,  Mbunge David Kihenzile akihitimisha hoja na majumuisho ya Mikutano hiyo aliiangukia  Serikali iingilie Kati jambo hilo mara moja ili dhamira Serikali kushusha bei iweze wanufaisha wananchi wa Mufindi na Watanzania kwa ujumla.

"Mbolea kwetu haipatikani ndio changamoto kubwa, naomba serikali isaidie kupatikana, tunachangamoto kubwa sana, imekua ni kero zaidi licha ya kwamba serikali ilitoa ruzuku lakini mbolea haipatikani. " Amesema Kihenzile.

Kilio hicho, ni mwendelezo wa vilio kutoka maeneo mbali mbali nchini ambapo wakulima wamekua wakilalamikia kutopatikana kwa mbolea hiyo au kuuzwa kwa bei kubwa licha ya bajeti ya kilimo  kuongeza kutoka Shilingi Bilioni 340 kwa Mwaka 2021/2022 hadi kufikia zaidi ya Shilingi Bilioni 800.

 Serikali chini ya Rais  Dk Samia Suluhu Hassan  iliidhinisha shilingi bilioni 150 kutumika kwa ajili ya ruzuku ya mbolea ili kuwezesha upatikanaji wa bidhaa hiyo kwa wingi na kwa gharama nafuu.

Utoaji wa ruzuku ya mbolea kwa wakulima unalenga kuongeza uzalishaji wa chakula nchini na hivyo kuwa na usalama wa chakula na kukidhi upatikanaji wa malighafi za viwanda vya ndani.

Hadi kufikia  Agosti 31, 2022 wakulima 956,920 wamesajiliwa kwa ajili ya kupata mbolea ya ruzuku ambapo jumla ya tani 60,882 za mbolea zimenunuliwa na wakulima katika mikoa  mbali mbali nchini.

Aidha, Kihenzile amesema katika mkutano huo, Viongozi hao pamoja na kukubaliana kila Tawi kukamilisha Mpango Kazi na Vipaumbele vya Tawi na Kata,  pia wameomba Chama Cha Mapinduzi vitendea kazi mbali mbali ikiwemo  baiskeli, katiba ya Chama, simu janja kwa ajili ya Mawasiliano, bendera, kuongezewa posho kwa Watendaji na Mabalozi.

Pia, wameomba kupatiwa kadi za elektroniki pamoja na kadi za kawaida za Chama, lengo ni kupata wanachama wengi ili wapate fursa ya kushiriki chaguzi za mwakani pamoja na uchaguzi Mkuu 2025.

Aidha, Kihenzile amesema viongozi hao pia wameishukuru  Serikali ya CCM kwa ujenzi wa barabara ya Sawala Luhunga km 30 sambamba na kukubali kumalizia kipande kilichobaki cha kilometa 10 kwenda Iyegea.

" Lakini zaidi wamefurahishwa sana Serikali yao kwa mara ya kwanza kupitisha bajeti ya ujenzi wa  kiwango cha lami cha  barabara za Mafinga-Mgololo Kilometa 78 na Nyololo-Mtwango Kilometa 40.4."Amesema Kihenzile na kuongeza 

"Wamehisii  Serikali kuanza ujenzi wa barabara hizo Mara moja kwani imekuwa kero kubwa sana."Amesema 

Amesema viongozi hao wameishukuru Serikali kuanza kufanyia Usanifu wa kina na upembuzi yakinifu kwa barabara za Nyololo-Kasanga- Nyigo na Mgololo- Makambako na  wamepongeza kwa miaradi ya Maji ambayo imeanza kutekelezwa kwenye Kata za Mtwango, Makungu, Kiyowela, Idete, Igowole, Mninga, Malangali, Maduma, Idunda na Ihowanza. 

Amesema,  wamepongeza pia  Miradi ya Maji iliyopitishwa inayotajarajiwa kuanza hivi karibuni kwenye Kata za Nyololo, Mbalamaziwa na Itandula na  kuomba Kata ambazo hazijafikiwa kabisa zitazamwe ikiwemo Kata ya Mtambula, Luhunga  na Vijiji vingine ambavyohavijafikiwa. 

"Viongozi hao wa CCM wamefurahishwa sana na Mpango wa Serikali kuanza Ujenzi wa Chuo cha Ufundi Stadi VETA, sambamba na kuanza ujenzi wa Kiwnada cha Parachichi Kata ya Nyololo ambapo ilipangwa kujengwa Makao Makuu ya Halmashauri kabla haijaamishiwa Itulavanu Kata ya Ikongos jambo ambalo kwa muda mrefu liliacha malalamiko kwa wananchi.

 Pongezi za dhati pia zimetolewa kwa Serikali ya CCM kupitisha Miradi kwenye Jimbo lao hususan ujenzi wa  vituo vipya vya afya, ujenzi shule ya Sekondari, ujenzi wa madarasa na miundombinu ya shule na sekta zingine.

Kipekee wametumia nafasi hiyo Kumshukuru Mbunge wao na Serikali yao kwa Mradi wa Shilingi bilioni 1.5  unaofadhiliwa na Shirika la Wolrd Vision wa Animal Gift wa Ugawaji Ng'ombe 600, Nguruwe 600 na Kuku 4,000 ambapo tayari wananchi wa Kata za Nyololo na Maduma kama Pilot Area wameanza kugawiwa  Mifugo hiyo. 

Ugawaji wa wanyama hao ni sehemu ya maono ya ambunge Kihenzile kwenye Utekelezaji wa falsafa ya 'One family, one catle' ambapo anaamini kila familia ikiwa na mfugo mmoja itaongeza uchumi, kupunguza utapiamlo na samadi itasaidia kwenye Kilimo.

Aidha badala ya kulima kwenye vinyungu mazao yaliyozoeleka wananchi watalima nyasi ambazo watakata na kupata malisho huku wakihifadhi vyanzo vya maji. Wajumbe hao waliojawa na sura za furaha na shukrani kwa Mbunge wao wameomba maeneo yenye changamoto yafanyiwe kazi ili wananchi wazidi kufurahia Serikali yao.

"Kwa mara ya kwanza barabara za lami za Mufindi zimepitishwa baada ya miaka 60 ya uhuru, kwao ni jambo jipya, hivyo wameshauri ujenzi uanze mara moja ili barabara hizo ziweze kuhudumia watu waliowengi, na zipo maeneo ya uchumi kwani kuna viwanda zaidi ya 15 na mashamba ya Mazao ya Biashara na Chakula ikiwemo Chai, Mahindi nakadhalika  na sehemu kubwa ya mabilioni ya fedha yanakusanywa kutoka Mufindi kama sehemu ya Kodi ya serikali yetu." Amesema Kihenzile 

Awali, akizungumza, Mwenyekiti wa UVCCM  Wilaya, Christian Mahenge alisema itakua ni ajabu mtu kutoka kutafuta jembe, alinoe wakati jembe tayari wanalo, wao kama Umoja wa vijana wanamuunga mkono Kihenzile kwenye kazi zake hata uchaguzi ujao 2025.

Kwa upande wa Mjumbe wa Kamati ya Siasa, Thomas Chonya alisema anamuona Kihenzile kama Mtendaji anatafsiri maoni kutoka kwenye makaratasi na kuyaweka kwa vitendo na kumuomba Mbunge wao  kadri apatapo rasilimali aweze kuwakutanisha ili wapate fursa kujadili kwa kina mafanikio na changamoto za Jimbo lao.

Kikao hicho kiliudhuriwa na viongozi mbali mbali wa matawi 79, pamoja na viongozi wastaafu akiwemo aliywahi kuwa Mwenyekiti wa Halmashauri Wilaya ya Mufindi na Diwani Kata ya Kiyowela kwa miaka 30 Peter Tweve, Mzee Kaguo aliyewahi kuwa Mwenyekiti wa CCM, Makamu Mwenyekiti wa Halmshauri na Diwani wa Kata ya Makungu miaka 21 ambapo viongozi wote hao walipongeza kazi nzuri iliyofanywa Mbunge Kihenzile.

Kikao hicho kilitanguliwa na Vikao vya Chama Ngazi ya Kata ambapo Madiwani walikutana Desemba 30, Ukumbi wa Kangesa, Mafinga Mji na  Desemba 31 kukutanisha Wenyeviti, Makatibu na Makatibu wenezi kwenye Kata zote za Jimbo la Mufindi Kusini. 















Share To:

Post A Comment: