Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt.Philip Mpango akizungumza na waumini wa Parokia ya Parokia ya Yohane Bosco iliopo Miyuji mkoani Dodoma mara baada ya Ibada ya Misa takatifu ya Jumapili ya Mwaka Mpya leo tarehe 1 Januari 2023.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt.Philip Mpango pamoja na mkewe Mama Mbonimpaye Mpango leo tarehe 1 Januari 2023 wameungana na waumini wa Kanisa Katoliki Parokia ya Yohane Bosco iliopo Miyuji mkoani Dodoma katika Ibada ya Misa takatifu ya Jumapili ya Mwaka Mpya. Ibada hiyo imeongozwa na Padre Innocent Nzavo.
Akizungumza mara baada ya ibada hiyo Makamu wa Rais amewaasa watanzania kuendelea kudumisha amani hususani kwa kutenda haki katika familia ikiwemo kulinda haki za wanawake wanaokabiliwa na changamoto za ukatili.
Amesema bado wanawake wanakabiliwa na dhuluma mbalimbali ikiwemo kupoteza mali pamoja na kunyimwa haki za ardhi.
Makamu wa Rais amesisitiza familia kuishi kwa amani katika mwaka 2023 ili kujiepusha na changamoto mbalimbali ikiwemo masuala ya ukatili.
Amewasihi watanzania kuendelea kuliombea Taifa amani ili kila mmoja aweze kuishi salama.
Pia Makamu wa Rais ametoa wito kwa kwa waumini kujenga amani na mazingira ili kutokuharibu kwa utupaji taka ovyo pamoja na ukataji miti.
Halikadhalika amewaasa watanzania kutumia wakati huu ambao mvua zimeanza kunyeesha kupanda miti katika maeneo yao.
Makamu wa Rais amewasihi viongozi wa dini na waumini kwa ujumla kuwaombea viongozi wa nchi ili waweze kuongoza vema kwa hekima ya Mungu na kwa maslahi ya taifa.
Post A Comment: