Mbunge wa Viti Maalumu Mkoa wa Mbeya na Naibu Waziri wa Maji, Mhandisi Maryprisca Mahundi amewataka wananchi wa mkoa huo kuwapeleka wagonjwa wa fistula katika Kambi ya matibabu ya ugonjwa huo inayoendelea katika Hospitali ya Kanda ya Rufani Mbeya kitengo cha wazazi Meta ili waondokane na fedheha inayowakabili.
Ameyasema hayo wakati wa uzinduzi wa Kambi hiyo iliyoandaliwa kwa ushirikiano kati ya Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Mbeya, Chama cha Madaktari wa upasuaji wa Fistula nchini na Mbunge huyo.
Amesema ugonjwa huo huwa unawasababishia maumivu makali wanawake huku ukiwaathiri pia kisaikolojia hasa pale wanaponyanyapaliwa na jamii pamoja na kukimbiwa na wenza.
Amesema tangu kambi hiyo ilipoanza Januari 16 mwaka huu mpaka sasa ni wanawake 15 pekee ndio waliofanyiwa upasuaji kati ya 60 wanaolengwa kunufaika na ofa hiyo.
Mwakilishi wa Chama cha Madaktari wa Upasuaji wa Fistula Tanzania, Dk. Peter Majige amesema wanawake 3000 huugua kila mwaka ugonjwa huo nchini huku 1500 pekee wakitibiwa kutokana na matatizo mbalimbali.
Amesema matibabu ya ugonjwa huo huwa yana gharama kubwa hali ambayo wananchi wengi huwa wanashindwa kumudu na hivyo kukilazimu chama hicho kuomba ufadhili kutoka kwenye mashirika mbalimbali ya kimataifa.
Ameiomba serikali kusamehe baadhi ya gharama za matibabu ya ugonjwa huo ili kuwasaidia wagonjwa wengi zaidi kupata matibabu na kuondokana na tatizo hilo.
Kaimu Mkurugenzi wa Hospitali ya Kanda ya Rufani ya Mbeya, Dk. Francis Rwegoshora amesema hospitali hiyo inatoa huduma ya matibabu ya ugonjwa huo lakini wagonjwa wengi wanashindwa kufika kutokana na uchumi mdogo pamoja na kutopata taarifa.
Amesema kambi hiyo iliyopelekwa katika hospitali hiyo itasaidia kuwayatambulisha matibabu hayo kwa wananchi wa maeneo mbalimbali ya mikoa ya Kanda ya Nyanda za Juu Kusini ili waende wakatibiwe.
Post A Comment: