Na John Walter-Babati
Madiwani wa Halmashauri ya Mji wa Babati mkoani Manyara wamepitisha mapendekezo ya mpango wa bajeti kwa mwaka wa fedha 2023/2024 kiasi cha fedha Sh.bilioni 29.9.
Wamepitisha mapendekezo ya bajeti hiyo leo januari 25, 2023 kwenye kikao maalumu cha Baraza la Madiwani kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa halmashauri hiyo, huku wakisisitiza kasi ya ukusanyaji mapato iendelee pamoja na kubuni vyanzo vipya.
Kaimu mkurugenzi wa Halmashauri ya mji wa Babati Anna Fissoo awali akisoma taarifa ya mapendekezo ya mpango huo wa bajeti wa mwaka wa fedha amesema wanatarajia kukusanya, kupokea na kutumia jumla ya shlingi Bilioni 29, 924,647,525.43 kutoka katika vyanzo vya ndani na Ruzuku toka serikali kuu na wadau wa maendeleo ikiwemo shilingi bilioni 18,222,831,421.43 za mishahara, shilingi Milioni 647,383,000 za matumizi mengineyo, shilingi Bilioni 2, 542,452,000 Ruzuku ya miradi ya maendeleo toka serikali kuu, Shilingi bilioni 5,993,027,000 Ruzuku ya Miradi ya maendeleo toka kwa wafadhili na shilingi bilioni 2,518,954,104 toka vyanzo vya ndani vya Halmashauri.
Kaimu Mkurugenzi , amesema wataendelea kusimamia nidhamu kwenye ukusanyaji wa mapato ya ndani, pamoja na kufuatilia vyanzo vipya.
Nao Madiwani wakichangia mapendekezo hayo ya mpango wa bajeti wa mwaka wa fedha 2023-2024 wamepitisha bajeti hiyo huku wakishauri kasi ya ukusanyaji mapato iendelee.
Aidha wamewapongeza watumishi wa Halmashauri hiyo kwa kujituma kwenye ukusanyaji wa mapato ya ndani.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Halmashauri ya mji wa Babati Addulrahmani Kololi, amewasihi watumishi kushirikiana na madiwani na watendaji wengine wa Halmashauri kushirikiana kuhakikisha wanatimiza wajibu wao kila mmoja ili kufanikisha zoezi la ukusanyaji wa mapato.
Post A Comment: