Na Dotto Mwaibale, Singida
KATIBU Mkuu wa Jumuiya ya Wazazi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa, Gilbert Kalima, ametoa rai kwa wazazi kujikita katika jukumu la kutoa elimu kwa jamii kuhusu suala la maadili kutokana na hivi sasa kuanza kujitokeza mfululizo wa matukio ya unyanyasaji wa kijinsia hapa nchini.
Akizungumza leo na wananchi,wanachama na viongozi wa CCM Wilaya ya Singida, amesema suala la malezi ya watoto ni jukumu la Jumuiya ya Wazazi kwani hivi sasa kumeanza kujitokeza mwenendo usiofaa kwa jamii katika nchi yetu.
"Kila tukikaa ndani ya siku mbili ukisikiliza vyombo vya habari wanakwambia kuna unyanyasaji wa kijinsia, mara utasikia baba kamuua mama,mara mama kauawa na mtoto au mama kaua mtoto au baba kampiga mama kipigo kikubwa,yote haya ni ukiukwaji wa maadili ambayo Jumuiya ya Wazazi inayakemea," amesema Kalima.
Kalima amesema Jumuiya ya Wazazi imeanza programu na msisitizo katika mambo mawili ambayo ni mafunzo na suala la kuimarisha uchumi wa jumuiya.
Amesema mafunzo ya kutosha yakifanyika viongozi watajua wao wa nini wanapaswa kulifanya badala ya hivi sasa ambapo inawezekana viongozi wanaochaguliwa wanakuwa hawafahamu majukumu yao.
"Leo hivi inawezekana Katibu wa Tawi amechaguliwa lakini hajui Kamati ya Utekelezaji inatakiwa ikutane mara ngapi kwa mwaka lakini baada ya mafunzo kufanyika kila kitu kitakwenda vizuri," amesema.
Kalima amesema Jumuiya ya Wazazi ikiwa imara maana yake chama, Jumuiya ya Vijana na Jumuiya ya Wanawake nayo itakuwa imara kwasababu Jumuiya ya Wazazi ni jumuishi na ni kiongozi wa jumuiya zote.
Amesemasema CCM ni chama imara ambacho kina muundo mzuri wa kiuongozi na ndio maana hivi karibuni vyama vya ukombozi Afrika ambavyo CCM ilivisaidia vilifika hapa nchini kujifunza kwasababu vinatambua CCM ni mwalimu wao kimuundo.
Aidha, Katibu Mkuu huyo amesema serikali ihakikishe inaweka mkazo mabasi ya shule wahudumu wawe wanawake badala ya wanaume kwani imebainika nako kumekuwa na vitendo vya unyanyasaji wa kijinsia kwa watoto.
Kuhusu mpango wa Bima ya Afya kwa wote, alisema CCM na serikali yake ina nina ya kuhakikisha kila ila mwananchi anapata huduma za afya hivyo wananchi wajitokeze kwa wingi kushiriki katika mpango huo.
Kalima aliitaka Serikali kukataa misaada inayotolewa na wafadhili yenye masharti ya kutaka serikali kuruhusu vitendo vya mapenzi ya jinsia moja.
" Tunaiomba serikali yetu tunajua,tumeshaona na tumesikia kuna baadhi ya misaada inayotolewa yenye masharti magumu masharti ambayo yanataka kuelekeza nchi ijikite kwenye mapenzi ya jinsia moja Jumuiya ya Wazazi inashauri ikibaini misaada yenye masharti kama hayo ikatae sababu siyo mipango ya Mungu bali ni laana," alisema.
Kalima alisema hivi karibuni alisoma mahali fulani wanajiandaa kutengeneza mitaala katika shule za swali na msingi kuanza kuwafundisha watoto masuala ya ushoga.
Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Singida, Martha Mlata, akizungumza kwenye mkutano huo.
Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi wa CCM Mkoa wa Singida, Bertha Nakomolwa, akizungumza kwenye mkutano huo. |
Post A Comment: