Na John Walter-Manyara
Mkurugenzi wa Kampuni ya Mati super Brands Ltd David Mulokozi amesema miaka mitano ya kampuni hiyo anajivunia kuajiri watu zaidi ya 390.
Licha ya kampuni hiyo kuisaidia serikali kupunguza tatizo la ajira, lakini pia kwa kiasi kikubwa imesaidia kupunguza uhalifu mbalimbali mtaani na kuchochea fursa za Maendeleo hapa nchini.
Mati Super Brands Limited ni miongoni mwa kampuni zinazolipa kodi kwa wakati serikalini.
Mwaka 2022 Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ilitambua mchango wa walipa kodi bora kwa kutoa tuzo maalum za pongezi ambapo Mati Super Brands Limited ilipongezwa na kupewa cheti kwa kushika nafasi ya pili.
Kampuni hiyo inalipa mabilioni ya fedha kama kodi serikalini na kuwalipa wafanyakazi wake mishahara kwa wakati.
David Mulokozi pia ni Makamu mwenyekiti wa viwanda (TCCIA) mkoa wa Manyara, anasema fursa za biashara anapoziona huwa hachelewi lazima azifanyie kazi haraka.
Amesema hayo kwenye usiku wa kuuaga mwaka 2022 na kuupokea mwaka 2023 hafla iliyofanyika kiwandani hapo mtaa wa Korongo mbili Mjini Babati usiku wa kuamkia January 1,2023.
Hafla hiyo ilihudhuriwa na watu mbalimbali wakiwemo wananchi wa Babati na Viongozi wa serikali.
Mlokozi amesema anaamini hawezi kuwa bilionea bila wafanyakazi ambao wanaumiza kichwa kuhakikisha bidhaa za Mati zinauzika kila pembe.
Pamoja na hayo wameitambulisha makala maalum inayozungumzia kampuni hiyo tangu kuanzishwa kwake na mafanikio yaliyopatikana mpaka sasa.
Ndani ya makala hiyo imemzungumzia mwanzilishi na mtoa wazo wa kiwanda cha kuzalisha pombe Kali kinachoitwa Mati super Brands Limited, David Mulokozi aliyezaliwa wilaya ya Mbulu mkoani Manyara zaidi ya miaka 40 iliyopita.
Katika makuzi yake David Mulokozi alifanikiwa kupata elimu kwa ngazi ya Msingi, Sekondari pamoja na vyuo mbalimbali hapa nchini Tanzania na nje ya nchi.
Baada ya kufanikisha kujaza maarifa ya kutosha kichwani mwake akaamua kuyawekeza kwenye ndoto zake za muda mrefu za kuwa mfanyabiashara mkubwa wa kuzalisha vinywaji aina ya pombe kali ikiwa ni sehemu ya kutimiza ndoto za babu yake aliyekuwa akifanya Biashara hiyo enzi za uhai wake kwa utaratibu usio rasmi.
Na sasa Mati super Brands limited ndani ya muda mfupi wa miaka mitano, imefikia mafanikio makubwa kiasi Cha kuajiri wafanyakazi wengi walio katika mfumo rasmi pamoja na kutoa misaada mbalimbali kwa jamii haswa wenye mahitaji maalum ikiwa ni mipango mahususi ya kampuni.
Kinachofanywa na Kampuni ya Mati Super Brands ni utabiri uliofanywa na babu yake Damian Mulokozi aliyefahamika kwa jina la Jackson enzi za uhai wake hivyo yanayoendelea sasa ni utekelezaji wa maono na utabiri wa babu.
Siri ya kupata mafanikio yote hayo ni kujituma, uvumilivu, heshima, na kuishi watu vizuri kwa upendo, alisema David Mulokozi mkurugenzi wa Mati Super Brands Ltd.
Amesema changamoto zinazotokea ndizo zinazochangia kumsogeza mbele zaidi katika mafanikio na alizitumia kama fursa.
"Nilipopata changamoto marafiki wengi niliokuwa nao walinikimbia" David Mulokozi.
Mkurugenzi David Mulokozi katika hafla ya kuuaga mwaka 2022, alitangaza kuwaongezea mshahara wafanyakazi waliofanya kazi kwa kujituma zaidi mwaka 2022 ambao ni Aquiline Makoy, Japheth Kisanga, Florida, Amon Frank, Mhandisi Reginald Antony, Brayton Mnene, Doreen Themu, Mussa Massawe, David John, na Melania Stephane.
Kupitia Mulukozi tunapata funzo kubwa kwamba tuishi ndoto zetu bila kujali tunapitia changamoto au vikwazo gani katika maisha yetu ya kila siku.
Mpaka sasa Mati super Brands Limited inazalisha na kusambaza vinywaji, pombe kali aina ya Strong Dry Gin, Sed pineapple Flavour Gin, Strong Coffee na Tanzanite premium vodka.
Post A Comment: