Kamanda wa jeshi la Polis mkoa wa Tanga Henry Mwaibambe akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kufanya usafi katika soko la samaki la Deep Sea lililopo jijini Tanga wakishirikana na halmashauri ya jiji, wafanybiashara na wavuvi wa samaki leo January 24,2023..
Jeshi la Polisi la mkoa wa Tanga kwa kushirikiana na halmashauri ya jiji la Tanga limeungana na wananchi ,wavuvi pamoja na wafanyabiashara wa samaki kufanya usafi wa mazingira katika soko la Deep see hii ikilenga kuhamasisha utunzaji wa mazingira na kuzingatia usafi ili kuepukana na magonjwa mbalimbali yakiwemo ya mlipuko.
Akizungumza kamanda wa jeshi la Polisi mkoa wa Tanga Henry Mwibambe amesema kuwa wamejipanga zaidi si kuimarisha tu ulinzi na usalama wa raia na mali zao pekee bali wamekuja na mpango kabambe kushirikiana na jamii ikiwemo kutoa msaada wa aina mbalimbali huku akiwataka wananchi kutokutumia eneo hilo kama magenge ya wahalifu .
"Jeshi la Polisi tumeamua tushirikiana na halmashauri ya jiji kufanya usafi wa mazingira tunafahamu asilimia kubwa ya samaki kwa jiji la Tanga wanapatikana katika eneo hili la Deep Sea kufanya usafi wa mazingira , eneo hili ni muhimu sana ninacho waomba wahusika wa eneo hili ni kwamba eneo hili lisewe la kulala mateja na vibaka tuendelee kushirikiana kuhakikisha eneo hili linazidi kuwa shwari"
"Huu ni mwanzo tu wa jeshi la Polisi mkoa wa Tanga tumejipanga kushiriikiana na jamii kutatua matatizo mbalimbali, tutaendelea kushirikiana na wananchi kufanya usafi katika maeneo mbalimbali kulingana na muda utakavyoruhusu"alisema Kamanda Mwaibambe.
"Sasa hivi duniani kote wimbo uliopo ni uhifadhi wa mazingira tumejisahau sasa hivi hali ya hewa imebadilika, suala la usafi wa mazingira ni la kila mmoja sio swala la mtu mmoja wote tushirikiane kutunza mazingira" alisistiza Kamanda huyo.
Afisa usafi na mazingira wa halmashauri ya jiji la Tanga Kizito Mkwabi amesema kuwa katika kusimamia na kuzingatia usafi wa mazingira katika eneo hilo la Deep Sea ambalo hutegemewa na wakazi wa jiji kwa ajili ya samaki ni muhimu kuimarisha usafi wakati wote akiwataka wakazi kuunga mkono juhudi za wadau kuwa na desturi ya kuweka jiji safi katika maeneo yao wanayoishi.
"Napenda kulipongeza kwa dhati kabisa jeshi la polisi mkoa wa Tanga na sisi tunaona hii ni fahari kwetu kwa kufanya tukio hili katika eneo la Deep sea ambalo ni muhimu sana kwa jiji letu ambalo linategemewa na jiji letu linalohusika na mfumo mzima wa chakula hili linasimamia usalama wa afya ya wananchi wa jiji la Tanga kupitia lishe na kila mmoja anatakiwa kutekeleza katika eneo alilopo na hili liwe ni mfano kwa wengine pia " alisema Mkwabi
Amesema kuwa licha ya jitihada zinazofanyika katika kuliweka jiji la Tanga katika hali ya usafi bado wapo baadhi ya wananchi ambao wamekuwa wakitupa taka ovyo hali ambayo inahatarisha usamala wao kiafya hivyo kuwataka kushirikiana kutoa elimu zaidi.
"Wakati tunapopambana kuweka jiji letu katika hali ya usafi bado kuna baadhi ya wananchi wanatupa taka ovyo na hili tunatakiwa kulidhibiti kwa pamoja hasa kutoa elimu kwa jamii kujua umuhimu wa kuzingatia usafi wakati wote kila mtu akifanya hivyo utakuta kesho jiji letu linakuwa safi kwa pamoja tukishirikiana tutafikia malengo"
Mwenyekiti wa mazingira katika soko hilo la Deep Sea Hamis Saidi amelipongeza na kulishukuru jeshi la polisi mkoa wa Tanga kujitokeza kufanya usafi katika eneo hilo wakiwa ni wadau wa mazingira akiomba ushirikiano huo uendelee baina ya wadau.
"Nashukuru sana kwa jeshi la polisi kushirikiana na wafanyabiashara pamoja na wachuuzi kufanya usafi wa pamoja wametupa hamasa na nguvu kubwa kwa pamoja tumejipanga kwa sababu tumepata fundisho la kutosha" alisema Said.
Post A Comment: