Naibu Waziri Ofisi ya Rais – TAMISEMI, Dk Festo Dugange amewataka viongozi wa Elimu ngazi ya Shule, Kata, Halmashauri na Mikoa kufuatilia mienendo ya ufundishaji na ujifunzaji shuleni kwa kushauriana na walimu na kuhakikisha wanafunzi wanapata umahiri uliokusudiwa katika masomo yote.
Dk Dugange ametoa maelekezo hayo Leo tarehe 9 Januari 2023 mkoani Njombe katika Mkutano wa tathmini ya utekelezaji wa shughuli za uboreshaji na usimamizi wa Elimu msingi na sekondari uliowakutanisha viongozi wa Elimu ngazi zote.
“Viongozi wa Elimu jielekezeni zaidi kufuatilia ufundishaji wa walimu darasani na kutatua kero za walimu kwenye maeneo yao ya kazi na mhakikishe mnaimarisha uwajibikaji wa watumishi wote katika ngazi zote ili kuongeza tija katika utendaji wa kazi” amesisitiza Dk Dugange.
Amewataka Walimu kujiwekea malengo yao binafsi katika masomo wanayofundisha na kuhakikisha hakuna mwanafunzi anayeshindwa kupata umahiri uliokusudiwa katika somo lake analofundisha.
Dk. Dugange amesem Rais Dk Samia Suluhu Hassan amefanya mambo makubwa na anaendela kuwekeza katika elimu ambapo ameendelea kutoa kiasi cha Shilingi Bilioni 29.82 kila Mwezi kwa ajili ya Elimu bila ada.
Aidha, Dk Dugange ameeleza Rais Dk Samia Suluhu Hassan ametoa Shilingi Bilioni 160 kwa ajili ya ujenzi wa madarasa mapya nchi nzima kwa ajili ya kupokea wanafunzi kidato cha kwanza mwaka 2023 ambao wameanza kupokelewa mashuleni leo.
Hadhalika, amesema Serikali inaendelea kuwekeza pesa nyingi katika Sekta ya elimu kupitia miradi mbalimbali kama mradi wa kuimarisha Elimu ya Sekondari SEQUIP wa Shilingi Trilioni 1.2, mradi wa kuimarisha Elimu ya Msingi BOOST wa Shilingi Trilion 1.15.
Wakati huo huo, Dk Dugange ameeleza mafanikio ya Katika Sekta ya Elimu ambapo idadi ya Wanafunzi wa elimumsingi wameongezeka kutoka wanafunzi 11,877,565 mwaka 2016 hadi 15,609,931 mwaka 2022 pia idadi ya wanafunzi wa kidato cha tano na sita iliongezeka kwa asilimia 35.86 kutoka 131,362 mwaka 2016 hadi 178,473 mwaka 2022.
Post A Comment: