Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo ya muda mfupi ya Mawakala wa Mali Zisizohamishika yanayofanyika kwenye Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE) Dar es Salaam tarehe 30 Januari 2023.

Sehemu ya washiriki wa ufunguzi wa mafunzo ya muda mfupi ya Mawakala wa Mali Zisizohamishika (MADALALI) yanayofanyika Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE) Dar es Salaam tarehe 30 Januari 2023.

Makamu Mkuu wa Chuo cha Elimu ya Baishara (CBE) Profesa Edda Lwoga akizungumza katika ufunguzi wa mafunzo ya muda mfupi ya Mawakala wa Mali Zisizohamishika yanayofanyika Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE) Dar es Salaam tarehe 30 Januari 2023.

Washiriki wa ufunguzi wa mafunzo ya muda mfupi ya Mawakala wa Mali Zisizohamishika (MADALALI) yanayofanyika katika Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE) Dar es Salaam wakifuatilia hotuba ya Waziri wa Ardhi Dkt Angeline Mabula tarehe 30 Januari 2023.

Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akisalimiana na viongozi wa Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE) alipowasili katika ufunguzi wa mafunzo ya muda mfupi ya Mawakala wa Mali Zisizohamishika tarehe 30 Januari 2023.

Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula (wa tatu kushoto waliokaa) akiwa katika picha ya pamoja na viongozi na watumishi wa Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE) alipokwenda kufungua mafunzo ya muda mfupi ya Mawakala wa Mali Zisizohamishika tarehe 30 Januari 2023. (PICHA ZOTE NA WIZARA YA ARDHI)

*****************************

Na Munir Shemweta, WANMM

Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula ameataka kutolewa mafunzo ya maadili kwa Mawakala wa Mali Zisizohamishika (MADALALI)

Dkt Mabula amesema hayo leo tarehe 30 Januari 2023 wakati akifungua Mafunzo ya muda mfupi ya Mawakala wa Mali Zisizohamishika (MADALALI) yanayoendeshwa na Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE) kwa kushirikiana na Chama cha Mawakala wa Mali Zisizohamishika (AREA) yanayofanyika jijini Dar es Salaam.

Alisema, pamoja na mafunzo yanayotolewa kuwa ya kitaalamu zaidi lakini upo umuhimu mkubwa wa kutolewa mafunzo yanayohusu maadili kwa kuwa eneo hilo limekuwa likisababisha malalamiko mengi kwa jamii.

Alitolea mfano wa Mawakala kuchukua kamisheni toka pande zote zinazohusika kwenye mauziano au upangaji nyumba na kubainisha kuwa suala hilo limekuwa kichocheo cha kupanda bei au kodi za nyumba na kuzidi viwango vya soko lengo likiwa kujipatia kamisheni kubwa na hivyo kuvuruga mwenendo wa soko la milki nchini.

Kwa mujibu wa Dkt Mabula, wapo Madalali wanaolalamikiwa kufanya vitendo vya utapeli ambapo huwadanganya wateja na kusababisha wateja hao kununua viwanja huku wakijua fika kuwa viwanja hivyo ni mali ya watu wengine na mwisho wa siku hujipatia fedha isivyo halali.

‘’Mafunzo kuhusu maadili ni muhimu sana kwa kuwa utendaji kazi unaozingatia suala hili la maadili utawezesha kujijengea heshima, kuaminika, kutoa huduma bora na hivyo kuwezesha kukua biashara na kujenga uaminifu kwa jamii waayoihudumia’’. Alisema Dkt Mabula

Alibainisha kuwa, katika baadhi ya nchi zikiwemo Kenya na Afrika kusini fani ya madalali inaheshimika na kuthaminiwa kwa kuwa imewekewa utaratibu wa usimamaizi na hivyo masuala ya uadilifu na weledi yanazingatiwa na kusimamiwa ipasavyo.

Alisema, Kenya inayo sheria ya usajili wa mawakala inayojulikana kama Estate Agents Act ya mwaka 1984 iliyorekebishwa mwaka 2012 huku Afirika Kusini ikiwa na sheria ya Property Prractitioners Act ya mwaka 2019 iliyounda mamlaka ya usimamaizi wa wataalamu wa masuala ya milki wakiwemo mawakala wa usimamizi wa mali zisizohamishika.

Alikipongeza Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE) pamoja na Chama cha Mawakala wa Mali Zisizohamishika (AREA) kwa kubuni mpango wa mafunzo unaoelenga kuhakikisha kuwa fani ya uwakala wa mali zisizohamishika inaendeshwa kitaalamu.

‘’Hatua hii mliyoichukua kuwafundisha vijana wajasiriamali wanaojishughulisha na shughuli zisizo rasmi ili kuingia katika utaratibu rasmi wa kufanya shughuli zao itawasaidia siyo tu kuwajengea uwezo wa kitaalamu bali pia kuwajengea kuajimini na kuaminiwa na jamii.

Amesema wizara yake iatatoa ushirikiano mkubwa ili kuhakikisha fani ya mwakala inaboreshwa ili shughuli za mawakala wa mali zisizohamishika ziweze kuanyuka kwa ufanisi na tija.

Mwenyekiti wa Chama cha Mawakala wa Mali Zisizohamishika (AREA) Erick Rweikiza amesema dhamira ya chama chake ni kuweka mazingira bora ya kuelimisha wanachama juu ya taaluma na kujenga umoja wa kibiashara pamoja na kutetea maslahi ya wanachama ili kuweka mazingira bora kwa wapangishaji, wauzaji na wanunuzi aliowaeleza kuwa ndiyo waajiri wa mawakala.

‘’Nia ni kuwafundisha wasio na ajira kujiajiri kupitia taaluma ya mawakala wa mali zisizohamishika’’ alisema Rweikiza.

Kwa upande wake Makamu Mkuu wa Chuo cha Elimu ya Bishara (CBE) Prof Edda Lwoga alisema, elimu inayotolewa na chuo chake kwa mawakala inatolewa chini ya mpango kabambe wa kuwafikia vijana wa kitanzania na kurasimisha shughuli zisizo rasmi zinazofanywa na jamii kubwa ya watanzania.

‘’Katika kutambua juhudi za serikali kwenye mpango wa kurasimisha taaluma ikiwa ni pamoja na kusajili mawakala sisi kama chuo tumejidhatiti na tuko tayari kushirikiana na serikali kwenye mchakato ikiwa ni pamoja na kutoa elimu kuhakikisha watendaji wana viwango vinavyokubalika kabla ya kuajiriwa’’. Alisema Profesa Edda Lwoga.
Share To:

emmanuel mbatilo

Post A Comment: