Naibu Waziri wa Madini Dkt. Steven Kiruswa ameiomba Benki ya Dunia kuwezesha kufanyika kwa tafiti za kina kwa nchi zenye utajiri wa Madini ya Kimkakati yanayohitajika kwa kiasi kikubwa kwa sasa duniani.
Amesema tayari nchi ya Tanzania imekamilisha tafiti za awali kwa madini hayo na kueleza kuwa, inacho kiasi kikubwa cha rasilimali hiyo ikihusisha madini ya Nickeli, Shaba, Cobolt, Vanadium, Kinywe (Graphite) Chuma, Liuthium, Rare Earth Element, Niobium na mengineyo.
Ameongeza kwamba, kutokana na uwepo wa utajiri huo wa kutosha, bado kunahitajika kufanyika tafiti za kina na hivyo kuiomba benki ya dunia kutoa fedha kwa ajili ya kuendeleza shughuli za utafiti wa madini hayo ili kuziwezesha nchi wazalishaji kujua kiasi kilichopo cha madini hayo na hatimaye kuziwezesha nchi hizo kuwa na kanzidata ya madini hayo.
Dkt. Kiruswa ameyasema hayo Januari 10, 2023, wakati akichangia hoja katika Kongamano la Pili la Uendelezaji wa Madini ya Kimkakati unaofanyika katika jiji la Riyadh nchini Saudi Arabia.
Pia, ameiomba benki hiyo kuongeza ushirikiano kwa nchi wazalishaji katika kusaidia kuongeza ujuzi kwa wataalam katika masuala ya utafiti na uchimbaji wa madini ya kimkakati ambayo ndiyo hitaji kubwa la sasa duniani.
Awali, akifungua mkutano huo, Waziri wa Viwanda na Rasilimali Madini wa Saudi Arabia Mhe. Bandar Ibrahim Al Khorayef ameeleza umuhimu wa nchi za Afrika na Asia kushirikiana katika kusimamia shughuli za utafiti wa madini ya kimkakati ili yaweze kutumika kwa sasa na kuhakikisha yanazinufaisha nchi zenye rasilimali hizo na kukuza uchumi na maendeleo ya watu.
Kwa upande wake, Balozi wa Tanzania nchini Saudi Arabia Mhe. Jabir Mwadini ameipongeza Wizara kwa kushiriki katika kongamano hilo kutokana na utajiri wa rasilimali hiyo nchi iliyobarikiwa kuwa nayo ikiwemo madini hayo inayohitajika sana kwa sasa duniani na kueleza kuwa, ni fursa muhimu kwa taifa.
Aidha, Mhe. balozi Mwadini ameahidi kuendelea kutafuta wawekezaji ili waweze kuwekeza katika sekta za madini, utalii, uchumi wa buluu na kilimo.
Mkutano huo umehudhuriwa na Mawaziri na wawakilishi kutoka nchi 60 wa wizara za madini za Kanda ya Afrika, Mashariki ya Kati na Asia.
Miongoni mwa masuala muhimu yanayojadiliwa katika kongamano hilo ni pamoja na namna ya kuzalisha madini hayo pasipo kuchafua mazingira huku rasilimali hiyo ikitakiwa kuzinufaisha kiuchumi nchi wazalishaji.
Kwa upande wa Tanzania, Dkt. Kiruswa ameambatana na Balozi wa Tanzania nchini humo Mhe. Ali Mwadini, Kamishna Msaidizi anayeshughulikia masuala ya CSR na Local Content Maruvoko Msechu na Mjiolojia kutoka Wizara ya Madini Joseph Ngulumwa.
Post A Comment: