SPIKA wa Bunge la Tanzania, Dk Tulia Ackson ambaye ni Mbunge wa Mbeya Mjini, amewataka wananchi wa kata mbalimbali za Jiji la Mbeya ikiwemo ya Ruanda kuwa mstari wa mbele kuzingatia usafi katika maeneo yao, ili kusaidia kulinda hadhi ya jiji.
Dk Tulia ametoa wito huo Januari 2, 2023 , wakati alipowaongoza wananchi wa Kata ya Ruanda kufanya usafi eneo la Umati, ambalo limekithiri uchafu kwa muda mrefu.
Dk Tulia pia amechukua fursa hiyo kuwaeleza wananchi hao kuhusu utaratibu mpya wa Jiji wa kuondoa maghuba katika mitaa na zoezi la uzoaji taka kuelekezwa katika kata husika.
Pia amemtaka Ofisa Mazingira Jiji la Mbeya, Nimrod Kiporoza kutokaa ofisini, badala yake apite katika kila kata kubaini changamoto za kuwepo taka.
Naye Mwenyekiti wa Mtaa wa Benki, Anna Ndimbwa amesema mara kadhaa amefuatilia uzoaji wa taka katika eneo hilo bila mafanikio licha ya taarifa kuziwasilisha kwa wahusika.
Kaimu Meya wa Jiji la Mbeya, Kefasi Mwasote licha ya kukiri kuwepo kwa uchafu katika kata nyingi ameahidi kusimamia jiji liwe safi.
Amesema katika vikao vya Baraza waliazimia usafi usimamiwe na wazabuni kupitia vikundi mbalimbali na kuyaondosha maghuba katika maeneo yote, ili taka zizolewe kwa muda maalumu kila kata kwa namna watakavyokubaliana.
Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi wa Jiji la Mbeya, Wakili Trifonia Kisiga, amesema watashirikiana na madiwani katika kila kata, ili kuhakikisha Jiji linakuwa na mazingira safi
Post A Comment: