Wakala ya Barabara Tanzania (Tanroads) mkoa wa Dar es Salaam imetangaza kulifunga Daraja la Tanzanite kwa siku nane kwa ajili ya maboresho ya kuwekwa nembo ya Tanzanite.

Kulingana na taarifa kwa umma iliyotolewa jana Jumamosi, Desemba 31,2022 na Tanroads daraja hilo litafungwa kuanzia kesho Jumatatu Januari 2, 2023 saa 12 asubuhi na kufunguliwa Januari 9, saa 12 asubuhi.

“Katika muda wote wa maboresho hayo, daraja hili halitatumika kwasababu za kiusalama hivyo Tanroads mkoa wa Dar es Salaam inawashauri watumiaji wa daraja kutumia barabara ya Kaunda na Ali Hassan Mwinyi,” imeelezwa kwenye taarifa hiyo.


Maboresho ya daraja hilo lenye nembo ya Mwenge wa Uhuru yanakuja kufuatia agizo la Rais Samia Suluhu Hassan alilolitoa Machi 2022 wakati akizindua daraja hilo na kuamuagiza Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa kubadilisha alama hiyo na kuweka alama ya madini ya Tanzanite kuendana na jina la daraja hilo.

“Niseme kidogo waziri ushauri nilioupata kutoka kwa wananchi, daraja hili tunaliita la Tanzanite lakini alama tuliyoiweka ni alama ya mwenge. Pamoja na kutambua mwenge ni tunu yetu adhimu wananchi wangependa sana kuona alama ya tanzanite pale ilipo alama ya mwenge ili liendane na jina la daraja hili,” amesema Rais Samia.

Daraja hilo limekuwa msaada mkubwa kwa wakazi wa Dar es Salaam kwa kupunguza foleni pamoja na kuwa kivutio cha utalii kwa wananchi ndani na nje ya Dar es Salaam.

Hadi kukamilika kwa daraja hilo gharama za ujenzi ni takribani Sh243 bilioni likifadhiliwa na Serikali ya Korea Kusini na kujengwa na kampuni ya ujenzi ya GS E&C, lilianza kujengwa mwaka 2018 na kuzinduliwa mwaka 2022.

Urefu wa daraja hilo ni  kilomita 1.03, ikijumuisha  njia nne za magari na njia mbili za watembea kwa miguu, pamoja na  barabara unganishi zenye wa kilomita 5.2 na linaunganisha Hospitali ya Aga Khan na barabara za Obama, Kenyatta na Toures .

Share To:

Post A Comment: