TAASISI ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) iliyopo jijini Dar es Salaam kwa kushirikiana na madaktari bingwa kutoka India, imefanya upasuaji wa moyo wa tundu dogo na upasuaji mkubwa kwa watu 25 kwa siku sita.
Kaimu Mkurugenzi wa JKCI ,Dk Angela Muhozya akizungumza na waandishi wa habari leo, amesema upasuaji mkubwa unagharimu kiasi cha Sh milioni 16 ndani ya nchi, huku nje ni Sh milioni 40 kwa mgonjwa mmoja, ambapo wagonjwa 12 walifanyiwa.
Dk Muhozya amesema upande wa tundu dogo wagonjwa 13 walifanyiwa upasuaji, ambapo kwa mgonjwa mmoja gharama ni Sh milioni 29 na nje ya nchi ni Sh milioni 80 kwa mgonjwa mmoja.
“Kuazia tarehe 23 hadi 28 tumekuwa na madaktari kutoka India, lakini sasa tunaweza kufanya upasuaji wenyewe bila kusimamisha moyo, lakini kuna changamoto watu wengi wanakuja mioyo yao imeshachoka sana kiwango cha ufanya kazi wa moyo kimeenda hadi asilimia 25, tumempata mmoja ana kiwango cha asilimia 17 na upasuaji unakua mgumu na hatari,”amesisitiza.
Amebainisha kuwa madaktari hao wanaweza kufanya upasuaji hata kama kiwango cha hatari ni kubwa kwa sababu ya uzoefu na vifaa walivyonavyo.
“Wamefanyiwa upasuaji kwa ufanisi mkubwa na pia madaktari wameweza kujifunza wawahudumie vipi na tunajivunia kwani mashine hiyo kwa Afrika Mashariki iko sehemu mbili na tumeshajua jinsi ya kutumia na tunafanya upasuaji kwa wagonjwa ambao hawako viwango vya juu,” amesema.
Post A Comment: