Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Mashimba Ndaki, akizungumza na washiriki wa MafunzoRejea ya Maafisa Ugani wa Kanda ya Mashariki wakati akifungua mafunzo hayo yaliyofanyika mkoani Pwani jana Desemba 13, 2022.
Na Mbaraka Kambona, Pwani
WAZIRI wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Mashimba Ndaki amesema kuwa Wizara yake
imeanzisha vituo atamizi kuwawezesha vijana kufuga kwa tija ili kujikwamua
kimaisha na pia kuwa ni kichocheo kwa wafugaji wengine kujifunza kwa vitendo na
kubadilika kutoka katika ufugaji wa kienyeji na kufanya ufugaji wa kisasa
utakaowaletea tija zaidi na kupunguza migogoro isiyo ya lazima kati ya wafugaji
na watumiaji wengine wa ardhi.
Ndaki aliyasema hayo wakati akifunga Mafunzo Rejea kwa Maafisa Ugani wa
Kanda ya Mashariki yaliyofanyika mkoani Pwani jana Desemba 13, 2022.
Alisema kuwa Wizara yake imewekeza na inahamasisha Vijana kushiriki katika
uzalishaji wa mifugo kupitia Vituo Atamizi ambapo kwa mwaka wa fedha 2022/2023
vijana 240 waliohitimu vyuo vya Mafunzo ya Mifugo wamedahiliwa na kuanza
mafunzo ya unenepeshaji wa ng’ombe katika vituo nane (8).
“Kwa mantiki hiyo nawahimiza wadau mbalimbali kuwekeza na kuhamasisha
vijana kujiunga na Vituo atamizi ambavyo vimeanzishwa na Wizara kwa sababu
vijana hao wakimaliza mafunzo hayo watasaidia wafugaji wengine kubadilika na
kuanza kufuga kwa tija,” alisema Ndaki.
“Mwakani tunatarajia kuwa na vijana wengi zaidi kwa sababu tutaongeza
bajeti kuhusu vituo hivi ili tuweze kuwachukua vijana wengi zaidi hata kufikia
1000, kwa sababu vijana hawa wakitawanyika kote nchini wataleta mageuzi kwenye
ufugaji wetu,”alifafanua
Aidha, alisema kuwa huduma za ugani ni kiungo muhimu kati ya watafiti na
wafugaji ili kupata ufugaji wenye tija hivyo ni vyema maafisa ugani
wakaimarisha mahusiano mazuri ili waweze kufikia malengo tarajiwa.
“Nitoe rai kwenu kujenga ushirikiano madhubuti baina yenu na wafugaji
utakaowezesha kutoa taarifa sahihi, kusambaza teknolojia, kuelimisha, kutoa
ushauri wa kitaalamu na kupata mrejesho,”alisema.
Waziri Ndaki alisema kuwa wanatambua
changamoto mbalimbali zinazoikabili sekta ya mifugo hususan katika
utoaji wa huduma za Ugani hapa nchini lakini tayari Wizara kupitia Mpango wa
Mabadiliko wa Sekta ya Mifugo imebainisha mikakati na afua mbalimbali za
kuzipatia suluhisho changamoto hizo.
“Miongoni mwa juhudi za serikali ni pamoja na kuanza kutoa Mafunzo Rejea
kwa Maafisa Ugani Watakaowafundisha Wengine (Trainer of Trainee) ambapo jumla
ya Maafisa Ugani 800 watafikiwa kwa mwaka wa fedha, 2022/2023. Aidha, Wizara
inatarajia kutoa mafunzo elekezi kwa wafugaji 182,200 nchini ambapo ninyi
mtatusaidia sana katika kutekeleza jukumu hilo,”alifafanua.
Aliongeza kuwa katika kutatua changamoto ya ukosefu wa vitendea kazi vya kutolea huduma za Ugani, Wizara imepanga kununua pikipiki 1,200 ambazo zitaongeza chachu kama vitendea kazi muhimu katika Sekretarieti za Mikoa na Mamlaka ya Serikali za Mitaa. Vilevile Wizara imeanza matumizi ya mifumo ya TEHAMA (M-Kilimo na Digital Agricultural Service Portfolio (Ugani Kiganjani) kwa lengo la kuwafikia wafugaji wengi na kutoa mrejesho wa kila kazi ambayo Afisa Ugani atakuwa ametekeleza katika eneo lake.
Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Mashimba Ndaki(kulia) akiongea na Katibu Tawala wa Mkoa wa Pwani, Bi. Zuwena Omary alipotembelea Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani muda mfupi kabla ya kwenda kufunga Mafunzo Rejea ya Maafisa Ugani Kanda ya Mashariki yaliyofanyika mkoani Pwani Disemba 13, 2022.
Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Mashimba Ndaki (katikati) akimsikiliza Mkurugenzi wa Idara ya Utafiti, Mafunzo na Huduma za Ugani, Dkt. Angello Mwilawa (kulia) wakati akiagana na Mkurugenzi huyo punde baada ya kufunga Mafunzo Rejea ya Maafisa Ugani Kanda ya Mashariki yaliyofanyika mkoani Pwani Disemba 13, 2022. Kushoto ni Mkuu wa Wilaya ya Kibaha, Mhe. Sara Msafiri.
Post A Comment: