Na Mathias Canal, WEST-Dodoma
Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia imesema haina sababu ya kuagiza Vishikwambi kutoka nje ya nchi itaunga mkono jitihada za kampuni yoyote yenye nia ya kuanzisha kiwanda cha utengenezaji wa vishikwambi nchini.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Mhe Prof Adolf Mkenda amesema hayo Jijini Dodoma wakati alipokutana na Ndg Tosk Hans ambaye ni Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya TANZTECH ELECTRONICS LIMITED ya Jijini Arusha ambayo imedhamiria kuanza uzalishaji wa vishikwambi ndani ya nchi kwa ajili ya matumizi ya wanafunzi.
Kampuni hiyo tayari ina eneo Jijini Arusha kwa ajili ya kuanza uzalishaji wa vishikwambi na wataanza uzalishaji wa baadhi ya vifaa kama vile betri, na Cover huku wakiwa na program ya kuanza kuwafundisha watanzania mambo ya Uhandisi Electroniki.
Waziri Mkenda amesema kuwa kampuni yoyote itakayokuja nchini na utaratibu na masharti hayo aliyoyaweka ambayo ni kampuni kuanzisha Programu ya haraka ya baadhi ya vifaa kuanza kuunganishwa na kuzalishwa hapa nchini pia kampuni kuandaa programu ya kufundisha wanafunzi uhandisi Elekroniki, basi Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia itaunga mkono na kuipa kazi kwa ajili ya ununuzi wa vifaa hivyo.
“Tukipata kampuni kama hii ambayo itaanzisha uzalishaji wa Tablets nchini basi tutaacha kuagiza nje badala yake tutanunua kwao” Amesisitiza Waziri Mkenda
Pamoja na masharti hayo pia amesema kuwa masharti mengine ya msingi yatakayofanya Wizara yake kununua vishikwambi hivyo ni pamoja na ubora wa vishikwambi sambamba na bei rafiki kuliko kampuni zingine katika soko la Dunia.
Waziri Mkenda amesema kuwa hakutakuwa na upendeleo wowote kwa wale wanaotaka kuanzisha kuuza vishikwambi serikalini badala yake kampuni zenye uhitaji huo ni lazima zifuate masharti hayo aliyoyaweka.
Sambamba na hayo, Waziri Mkenda ameipongeza kampuni hiyo ya TANZTECH ELECTRONICS LIMITED kwa kukubali kufuata masharti ya Wizara ya Elimu iliyoyaweka kuanzisha kiwanda cha utengenezaji wa vishikwambi nchini.
Post A Comment: