Wakala wa Barabara nchini Mkoa wa Dodoma imetenga kiasi cha Shilingi bilioni 17.8 kwa ajili ya ujenzi wa barabara zenye jumla ya urefu wa Kilometa 1,707.02 ambapo utekelezaji wake unafanywa chini ya ufadhili wa Benki ya Dunia.
Hayo yamebainishwa katika kikao cha pili cha mwaka cha Bodi ya barabara kilichojadili utelekezaji wa miradi ya barabara za Mkoa chini ya mwenyekiti wake Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Rosemary Senyamule.
Akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa kazi kwa kipindi cha nusu mwaka Kaimu Meneja wa Wakala wa Barabara Mkoa Mhandisi Salome Kabunda amesema licha ya maendeleo mazuri ya utekelezaji wa miradi ya barabara katika Mkoa wa Dodoma bado kuna changamoto zinazoikabili Taasisi katika utekelezaji wake.
Amezitaja changamoto hizo kuwa ni pamoja na uvamizi wa wananchi kwa kujenga kwenye hifadhi za barabara, uswagaji wa mifugo barabarani, utupaji taka kwenye mifereji ya mvua na kusababisha mafuriko kutokana na kuziba kwa mifereji, ufinyu wa bajeti pamoja na uegeshaji holela wa magari unaopelekea uharibifu wa barabara.
Kwa upande wa Wakala wa ujenzi wa barabara Mijini na Vijijini TARURA, Meneja wa TARURA Mkoa wa Dodoma Mhandisi Lusako Kilembe amesema wamedhamiria kujenga barabara zenye urefu wa Km 7,504.94 pamoja na barabara zinazolisha barabara kuu zenye urefu wa Km 900.56.
“Jumla ya mikataba 67 ya utengenezaji wa barabara yenye thamani ya shilingi Bilioni 23.65 imeidhinishwa. Pia katika ujenzi wa Barabara hizi, matumizi ya teknolojia ya ECOROADS na POLYMER zimetumika ikiwa ni pamoja na matumizi ya mawe kwenye maeneo ambayo upatikanaji wake ni rahisi ili kupunguza matumizi ya saruji na nondo” Alisisitiza Mhandisi Kilembe.
Kikao hicho kimeazimia Wakala wa Barabara nchini kufuatilia utaratibu wa kuhamisha shule ya Unkunku iliyopo Kondoa Mji ili kupisha mradi wa barabara, kuidhinishwa ujenzi wa barabara ya Simanjiro – Kongwa, kujenga maegesho ya magari eneo la Chimulata Wilaya ya Kongwa na kutumia Sheria katika kudhibiti na kupambana na waharibifu wa miundombinu kwa kupitisha mifugo kwenye barabara.
Mwenyekiti wa kikao hicho, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Rosemary Senyamule ameiagiza TANROADS kutoa elimu kwa wananchi ya matumizi sahihi ya barabara hususan kwenye maeneo korofi ambayo wananchi hufunga barabara wakihitaji matuta hata katika barabara ambazo hazina uhitaji huo zaidi ya alama za barabarani tu ili kuzuia ajali.
Aidha amewataka wakala wa barabara TANROADS kutenga bajeti ya kufungua barabara ya kutoka Dodoma mpaka Ruaha kwa ajili ya kuchochea na kuvutia utalii, kuweka taa za usalama barabarani katika maeneo yanayohitajika na kusisitiza usimamizi madhubuti wa miradi yote ili iweze kukamilika kwa ubora na wakati.
Kikao hiki kimehudhuriwa na wajumbe wa bodi ambao ni pamoja na Katibu Tawala Mkoa wa Dodoma Bi. Fatuma Mganga, wakuu wa Wilaya zote saba za Mkoa wa Dodoma, Wenyeviti wa Halmashauri Nane za Mkoa, Wakurugenzi Watendaji wa Halmashauri, Wabunge, Viongozi wa Taasisi zinazohusika na ujenzi wa barabara (TANROADS na TARURA).
Post A Comment: