Na Mashaka Mhando

Muheza


KATIBU Mstaafu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Ibrahim Shemdoe, amezindua kitabu chake cha Maisha na Utumishi Ulioacha Alama, huku akitoa wito kwa wasomi waendelee kutoa vitabu kwa faida na maendeleo ya jamii.


Akizungumza wakati wa hafla ya uzinduzi wa kitabu hicho, kilichozinduliwa na Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Dayosisi ya Kaskazini Mashariki, (KKKT-DKMS) Dkt Msafiri Mbilu, Shemdoe alisema ipo dhana imejengeka kwa wasomi kwamba wakitoa vitabu kuelezea historia za maisha yao, watakufa.


"Kuna dhana potofu imejengeka miongoni mwa wasomi wengi wanafikiri ukiandika kitabu unakufa kesho au utakufa haraka," alisema Shemdoe.


Alisema hiyo ni dhana ambayo wasomi hasa wenye PhD na Maprofesa wamekuwa na hiyo kasumba ili wasieneze ule udhoefu wao na maarifa yao kwa wananchi jambo ambalo halina ukweli wowote.


"Wasomi wanasema ukiandika kitabu unakufa siyo kweli ni uongo mtupu, baba na mama yangu pamoja na ndugu zangu wamekufa lakini hawakuandika kitabu, huu ni upotoshaji ambao ni lazima upigwe vita," alisema.


Alisema upotoshaji huo ni kudhoofisha Watanzania ambapo nchini Nigeria wamepiga hatua kwasababu wasomi wao wameandika vitabu vinavyosaidia Taifa lao lakini nchini tunasoma vitabu vingi vilivyotungwa na wazungu.


Katika kitabu chake hicho kinachoitwa 'Maisha na Utumishi Ulioacha Alama' kimeandikwa kwa msaada mkubwa wa mwanaye wa watau Aloicia Shemdoe na kupigwa chapa na mumewe Joshua Mhingo.


Dibaji ya kitabu hicho chenye kurasa 110, imandikwa na Profesa John Kiango ambaye ameelezea kwa kina ya safari ndefu ya Mwalimu Ibrahim Shemdoe alivyoanza kusaka elimu hadi alipokuwa mtumishi wa mfano wa kuigwa.


"Kwakuwa nafasi yangu ya dibaji ni ndogo napenda kumaliza kwa kumpongeza mwalimu Ibrahim Shemdoe kwa kujijengea wasifu huu kwa gharama kubwa, ukipata watu watano wenye karama kama hawa katika wilaya nchi itapata Maendeleo," alisema.


Akitoa salamu katika hafla hiyo, Mkuu wa wilaya ya Lushoto Kalist Lazaro alimpongeza mwalimu Shemdoe ka kutoa kitabu hicho chenye wasifu wake akiwa hai maana watu wamezoea kusikia wasifu wa watu mbalimbali wakiwa wamekufa.


Mbunge wa Muheza Hamis Mwinjuma maarufu MwanaFA, alisema atanunua kitabu hicho na kumsaidia mwalimu Shemdoe kukitangaza kitabu hicho.


Awali akizindua kitabu hicho Askofu Dkt Mbilu alisema jamii iige mfano wa kuandika vitabu kwa watoto kuandika wasifu wa wazazi wao waliofanya vizuri kwa Taifa kwa faida ya vizazi vijavyo.


"Sisi Waafrika tumezoea kusimulia lakini kuandika vitabu kama hivi itasaidia kuhifadhi maandiko hayo yatakayodumu kwa mida mrefu," alisema.


Mwalimu Shemdoe alifanya kazi mbalimbali za umma ikiwemo kuwa Katibu wa CCM wa wilaya mbalimbali ikiwemo wilaya ya Muheza alikostaafu mwaka 1998. Hivi sasa ana miaka 84.

Share To:

Post A Comment: