Aliyekuwa Mkuu wa wilaya ya Hai, mkoani Kilimanjaro Lengai Ole Sabaya, amefikishwa tena katika Mahakama Kuu Kanda ya Arusha ambayo leo imepanga kutaja rufaa ya kupinga hukumu iliyomwachia huru yeye na wenzake waliokuwa wakikabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi.
Mbali na Sabaya wajibu rufaa wengine ni Enock Mnkeni, John Aweyo, Sylvester Nyegu, Jackson Macha na Nathan Msuya.
Sabaya amefikishwa mahakamani hapo leo Jumatano Desemba 21, 2022 saa 3:06 asubuhi.
Rufaa iliyokatwa na Mkurugenzi wa Mashitaka nchini (DPP) dhidi ya Sabaya na wenzake watano, inapinga hukumu iliyotolewa na Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha, iliyowaachia Sabaya na wenzake sita waliokuwa wakikabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi namba 27/2021 katika mahakama hiyo ya chini.
Hukumu hiyo ya mahakama ya chini ilitolewa Juni 10, 2022 na Hakimu mkazi Patricia Kisinda ambapo mbali na Sabaya wengine walioshinda kesi hiyo ni Mnkeni, Watson Mwahomange Aweyo, Nyegu, Macha na Msuya.
Aidha katika rufaa hiyo namba 155/2022 wajibu rufaa ni sita ambao ni Sabaya, Mnkeni, Aweyo, Nyegu, Macha na Msuya isipokuwa Mwahomange.
Rufaa hiyo inasikilizwa na Jaji Salma Maghimbi, ambapo Desemba 14, 2022 aliahirisha rufaa hiyo na kutoa amri kwa Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Kanda ya Arusha,kuchapisha kwenye magazeti tangazo la hati wito kwa wajibu rufaa wanne kwenye rufaa hiyo.
Jaji Maghimbi alitoa amri hiyo baada ya mawakili wa serikali kuomba mahakama itoe amri kwa Naibu Msajili, kutoa machapisho hayo kwenye magazeti kutokana na jitihada za kuwapatia hati za wito kufanyika bila mafanikio.
Jaji Maghimbi alisema kwa sababu haki ya kusiilizwa ni haki ya msingi kabisa kwenye maamuzi ya mahakama hivyo wajibu rufaa wote wanatakiwa kupewa haki yao ya msingi ya kusikilizwa kwa kupewa wito wa kuja mahakamani kama sheria inavyotaka.
Amri hiyo ya Jaji huyo imetokana na ombi la Wakili wa serikali mwandamizi, Abdallah Chavula aliieleza mahakama kuwa rufaa hiyo imepangwa kwa ajili ya kusikilizwa lakini waliopo mahakamani ni wajibu rufaa wa kwanza (Sabaya) na wa nne (Nyegu) huku wajibu rufaa wa pili, tatu, tano na sita wakiwa hawapo.
Alieleza kuwa wajibu rufaa wanne ambao ni Mnkeni, Aweyo,Macha na Msuya hawapo mahakamani kwa mujibu wa taarifa walizopata kutoka kwa Naibu Msajili Mahakama Kuu Kanda ya Arusha jitihada za kuwapatia wito wajibu rufaa ambao hawapo mahakamani zimefanyika bila mafanikio yoyote.
Post A Comment: